China na Sierra Leone zaahidi kufanya ushirikiano katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 11, 2024

FREETOWN - China na Sierra Leone zimeahidi kuimarisha ushirikiano katika kinga na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza ili kuboresha ustawi wa watu wa Sierra Leone katika kongamano kuhusu magonjwa ya kuambukiza yanayoibuka na yanayoibuka tena, iliyoandaliwa na Kituo cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa cha China, (China CDC) na Wizara ya Afya na Usafi wa Mazingira ya Sierra Leone katika Freetown, mji mkuu wa Sierra Leone siku ya Jumatano.

Kongamano hilo lilikutanisha kundi la wataalam, watafiti, wataalamu wa afya na watunga sera katika sekta ya afya.

Xu Jianguo, Msomi wa Taasisi Kuu ya Uhandisi ya China anayefanya kazi China - CDC, amesema kuwa magonjwa ya kuambukiza yanayoibuka na kuibuka tena ni changamoto kubwa kwa usalama wa afya na maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Sierra Leone na kwamba hali hiyo inahitaji mbinu ya kina na iliyoratibiwa kuunganisha ufuatiliaji, upimaji, matibabu, kinga na utafiti.

Xu amesisitiza ushirikiano wa kirafiki wa muda mrefu kati ya China na Sierra Leone katika afya ya umma, hasa katika Sierra Leone ilipokabiliana na mlipuko wa Ebola na janga la UVIKO-19 .

Kongamano hilo lililenga kuimarisha ushirikiano, uandaaji na njia za kukabiliana na changamoto hizi zinazojitokeza za afya, Xu amesema, huku akiongeza kuwa inalenga kuchangia juhudi zinazoendelea za kudhibiti magonjwa ya kuambukiza nchini Sierra Leone, hatimaye kuboresha afya na ustawi wa watu wake.

Charles Senessie, kaimu waziri wa afya wa Sierra Leone, amesema kuongezeka kwa matukio ya magonjwa kama vile homa ya Lassa nchini humo inasisitiza haja ya kuwa na mfumo wenye uangalifu wa huduma za afya, mifumo thabiti ya ufuatiliaji na hatua madhubuti za kuzuia kuenea kwake.

Senessie amehimiza ushirikiano mzuri kati ya Sierra Leone na washirika wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na China, ili kuimarisha uwezo wa kukabiliana na magonjwa hayo.

"Kupitia ushirikiano, uvumbuzi na kujitolea kwa pamoja kwa ustawi wa taifa letu, tunaweza kukabiliana na changamoto hizi na kujenga mustakabali mzuri wa Sierra Leone," kamimu waziri huyo amesema.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha