

Lugha Nyingine
Blinken ahitimisha ziara yake katika Mashariki ya Kati kwa mazungumzo nchini Misri juu ya mgogoro wa Gaza, vifo vya Wapalestina vyafika 23,469
![]() |
Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi (Kulia) akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken mjini Cairo, Misri, Januari 11, 2024. (Ikulu ya Misri/ Xinhua) |
CAIRO - Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amefanya mazungumzo siku ya Alhamisi na Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri katika mji mkuu wa Misri, Cairo wakati akihitimisha ziara yake katika Mashariki ya Kati kuhusu mashambulizi na uvamizi wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Huku mazungumzo hayo yakijiri, Wizara ya Afya yenye makao yake makuu mjini Gaza siku hiyo ya Alhamisi imetangaza kwamba idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza imeongezeka hadi 23,469.
Msemaji wa Wizara hiyo Ashraf al-Qedra amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba Jeshi la Israel limewaua Wapalestina 112 na kujeruhi wengine 194 katika muda wa saa 24 zilizopita.
Wakati wa mazungumzo hayo, Sisi alimfahamisha Blinken "juhudi za Misri za kuwasiliana na pande zote ili kufikia usimamishaji vita wa mara moja huko Gaza," pamoja na kuhakikisha mtiririko wa kutosha wa misaada ya kibinadamu katika Gaza, imesema taarifa ya Ikulu ya Misri.
Rais wa Misri amesisitiza haja ya kumaliza "majanga ya kibinadamu huko Gaza," na umuhimu wa kufikia suluhu ya haki na ya pande zote ya suala la Palestina, kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Kwa upande wake Blinken ameelezea shukrani za Mareakni kwa juhudi za Misri za kuimarisha amani na utulivu katika eneo hilo, huku Sisi akisisitiza shauku ya Misri ya kuendelea na uratibu na Marekani ili kudumisha usalama na utulivu wa kikanda.
Viongozi hao pia wamekataa wazo la kuhamisha Wapalestina kutoka kwenye maeneo yao, kudumisha mashauriano ya kina na kufanya juhudi za kuleta amani, kudhibiti hali na kuzuia kuenea kwa mgogoro huo.
Hii ilikuwa ziara ya nne ya Blinken katika Mashariki ya Kati tangu Israel ianze oparesheni yake kubwa ya kijeshi dhidi ya Gaza Oktoba 7, 2023, kujibu mashambulizi ya kushtukiza yaliyoanzishwa na Hamas kusini mwa Israel.
Blinken alianza ziara hiyo ya kikanda wiki iliyopita na ametembelea Uturuki, Ugiriki, Jordan, Qatar, Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Israel, Ukingo wa Magharibi, Bahrain, na hatimaye Misri.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma