

Lugha Nyingine
Burundi yafunga mpaka na Rwanda, ikiituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi
KIGALI - Burundi imesema siku ya Alhamisi kwamba imefunga mpaka wake na Rwanda, karibu wiki mbili baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kumshutumu jirani huyo kwa kuunga mkono waasi ambapo mwishoni mwa Desemba, rais huyo aliishutumu Rwanda kwa kuwapokea waasi wa RED-Tabara waliodai kuhusika na mashambulizi ya Desemba 22 katika eneo la mpaka kati ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kusababisha vifo vya watu 20 na wengine tisa kujeruhiwa.
"Tumefunga mipaka yetu na Rwanda," Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Umma wa Burundi Martin Niteretse amenukuliwa na vyombo vya habari vya Burundi akisema siku ya Alhamisi. Waziri huyo amesema nchi yake inasitisha uhusiano wa kidiplomasia na Rwanda, kufunga mpaka wao na kuwafukuza raia wa Rwanda.
Ikijibu hatua hizo, Ofisi ya Msemaji wa Serikali ya Rwanda imetoa taarifa Alhamisi jioni, ikisema inasikitika Burundi kufunga mpaka kwa maamuzi ya upande mmoja.
"Serikali ya Rwanda imefahamu kupitia ripoti za vyombo vya habari kuhusu uamuzi wa upande mmoja wa serikali ya Burundi kufunga tena mipaka yake na Rwanda. Uamuzi huu utazuia usafirishaji wa watu na bidhaa kati ya nchi hizo mbili, na unakiuka kanuni za ushirikiano na muunganisho wa kikanda za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” imesema taarifa hiyo.
Shutuma hizo za Rais Ndayishimiye zilitolewa katika kipindi cha moja kwa moja kwenye kituo kimoja cha redio nchini humo Desemba 29, ambapo Ndayishimiye alisema, "Wanachama wa kundi hili la waasi (RED-Tabara) wanahifadhiwa, kulishwa na kutunzwa na Rwanda. Wanapewa pesa na ofisi za kazi na nchi hiyo."
Hata hivyo, Rwanda ilikanusha shutuma hizo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma