

Lugha Nyingine
Tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa yaanza kujiondoa kutoka DRC
Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Christophe Lutundula (Kulia) akihudhuria mkutano na waandishi wa habari na Bintou Keita, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini DRC huko Kinshasa, DRC, Januari 13 , 2024. (MONUSCO/ Xinhua)
KINSHASA - Tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), inayojulikana kama MONUSCO, imeanza kujiondoa nchini humo, amesema Christophe Lutundula, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC ambapo kujiondoa huko kwa MONUSCO kutafanyika kwa awamu tatu, ikianza na kujiondoa kikamilifu kwa wanajeshi na polisi wa MONUSCO kutoka jimbo la mashariki la Kivu Kusini ifikapo Aprili 30.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumamosi baada ya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliomhusisha Lutundula na Bintou Keita, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Mkuu wa MONUSCO, awamu ya pili na ya tatu ya kujiondoa kwa tume hiyo itatekelezwa kutoka Kivu Kaskazini na Ituri, majimbo mawili yanayokumbwa na migogoro ya kivita, huku kukiwa na tathmini ya kina wakati wa mchakato huo.
“Tunapigania kujiondoa huko kuwe kamilifu kuanzia mwishoni mwa Desemba 2024,” amesema Lutundula.
"Baada ya miaka 25 ya uwepo wake, MONUSCO bila shaka itaondoka DRC kabla ya mwisho wa 2024," kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Desemba 19, 2023, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) lilipitisha kwa kauli moja Azimio nambari 2717, likiweka mpango mpana wa kujiondoa kutoka DRC ambao unajumuisha awamu tatu na kukabidhi majukumu kwa serikali hatua kwa hatua. Hata hivyo, UNSC bado haijaweka tarehe ya mwisho ya kujiondoa kikamilifu.
MONUSCO imekuwepo nchini humo tangu Mwaka 1999. Ni mojawapo ya operesheni kubwa na yenye gharama kubwa zaidi duniani, ikiwa na bajeti ya kila mwaka ya dola karibu bilioni 1 za Marekani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma