

Lugha Nyingine
Mkuu wa Kamisheni ya AU asisitiza suluhu ya mataifa mawili kumaliza mgogoro kati ya Israel na Palestina
Wajumbe wanaohudhuria Mkutano wa 47 wa Kawaida wa Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika wakipiga picha pamoja mjini Addis Ababa, Ethiopia, Januari 15, 2024. (Xinhua/Michael Tewelde)
ADDIS ABABA – Mkutano wa 47 wa Kawaida wa Kamati ya Wawakilishi wa Kudumu (PRC) wa Umoja wa Afrika (AU) umefunguliwa Jumatatu huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, huku Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat akisisitiza suluhu ya mataifa mawili ili kumaliza mgogoro kati ya Israel na Palestina.
Faki amesema wakati athari za mgogoro wa Russia na Ukraine zinazidi kuongezeka, mgogoro wa Israel na Palestina unaendelea huku ukiwa na athari zisizoelezeka, na kusababisha majanga ya kibinadamu na uharibifu wa mali.
"Dhamiri ya Afrika imetikishwa kutokana na maafa ambayo yametokea kutokana na mgogoro huo, nasisitiza kwa mara nyingine tena wito wetu wa kusimamishwa kwa mapigano kwa ajili ya huduma za kibinadamu na mashauriano ya jumuiya ya kimataifa ili kufikia suluhu ya mataifa mawili kumaliza mgogoro huko," amesema.
Huku akitilia maanani kuendelea kushambuliwa kwa makombora kwa raia wa Palestina na uharibifu wa njia zao za kuishi, Faki amekumbuka kuwa mgogoro huo umekuwa ukifuatiliwa na kujaliwa kwa kiasi kikubwa na Afrika kwa zaidi ya miaka 60.
Amesema kuwa suluhu ya kudumu inahitajika ili kuhakikisha kuishi kwa mapatano kwa mataifa yote mawili ili kuruhusu watu wao kuishi katika hali ya amani na utulivu.
Afrika nayo hajaacha kuguswa na migogoro pia, amesema mwenyekiti huyo, huku akibainisha matatizo ya usalama yanayoendelea nchini Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na maeneo mengine ya bara hilo, yanayoathiri amani, utulivu na maendeleo ya bara hilo.
Amesema Umoja wa Afrika unahitaji kwenda mbali ili kufikia lengo kuu la umoja huo, yaani amani, muunganisho na maendeleo ya Afrika.
Mkutnao wa PRC unafanyika chini ya kaulimbiu "Elimisha Mwafrika anayefaa kwa Karne ya 21: Kujenga mifumo ya himilivu ya elimu kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa elimu jumuishi, ya maisha yote, yenye ubora na yenye fursa husika ya kujifunza barani Afrika."
Mkutano huo utafuatiwa na Mkutano wa 44 wa kawaida wa Baraza la Utendaji na Mkutano wa 37 wa Kawaida wa Baraza Kuu la AU, kuanzia katikati ya Februari.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma