

Lugha Nyingine
Israel yasema mazungumzo ya kusimamisha mapigano kati yake na Palestina "yamepata maendeleo"
Shirika la Utangazaji la Israel limesema, mazungumzo yanayoendelea ya kusimamisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas la Palestina "yamepata maendeleo."
Ripoti hiyo iliyotolewa jana Jumatatu imesema, maendeleo hayo yamepatikana baada ya kuona mabadiliko katika msimamo wa Kundi la Hamas.
Ripoti hiyo imemnukuu afisa wa usalama wa Israel akisema, masharti ya Israel katika mazungumzo hayo ni pamoja na kuwaachilia Waisraeli wote waliochukuliwa mateka isipokuwa wanajeshi wa Israel, kusimamisha vita, kuwaondoa wanajeshi wa Israel katika maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza, na kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kiusalama wa Palestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Israel ilitarajia kupokea majibu ya kundi la Hamas kwa masharti hayo siku hiyo, lakini kutokana na operesheni kubwa za jeshi la Israel huko Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza, huenda jibu hilo likachelewa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma