China na Uganda zaahidi kupanua ushirikiano wenye manufaa halisi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 23, 2024

KAMPALA - Rais wa Uganda Yoweri Museveni siku ya Jumamosi alikutana na mwakilishi maalum wa Rais Xi Jinping wa China Liu Guozhong ambaye alihudhuria Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi zisizofungamana na Upande wowote (NAM) na Mkutano wa 3 wa Wakuu wa Nchi za Ushirikiano wa Kusini na Kusini huko Kampala, Uganda. Pande zote mbili zilibadilishana maoni kwa kina kuhusu uhusiano wa pande mbili.

Liu, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Naibu Waziri Mkuu wa China, aliwasilisha salamu za Rais Xi kwa Rais Museveni na kuipongeza Uganda kwa kuandaa vyema mikutano hiyo miwili.

Ameelezea shukrani zake kwa mchango uliotolewa na Uganda kwa ajili ya kuimarisha mshikamano na ushirikiano wa nchi za kusini za dunia nzima na amesifu mafanikio ya Uganda katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“China inatilia maanani sana kuendeleza uhusiano na Uganda na ingependa kutekeleza kwa pamoja maafikiano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili” Liu amesema.

Ametoa wito kwa pande zote mbili kusaidiana kithabiti, kutumia vizuri uwezo wa kifursa wa ushirikiano wenye manufaa halisi, kuimarisha mawasiliano na uratibu katika masuala ya kimataifa, na kuendeleza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.

Kwa upande wake Rais Museveni amemuomba Liu kufikisha salamu za dhati kwa Rais Xi. Alimkaribisha Liu na ujumbe wa serikali ya China kuhudhuria mikutano hiyo miwili na kuishukuru China kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha mikutano hiyo.

Rais Museveni amesema, Uganda ingependa kushirikana na China katika kuenzi urafiki wao wa jadi, kuungana mkono kithabiti katika masilahi ya msingi, kupanua ushirikiano wa kufuata hali halisi na kuimarisha ustawi wa watu wa nchi hizo mbili, na akitakia mafanikio makubwa zaidi katika maendeleo ya China. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha