

Lugha Nyingine
Mkutano wa 3 wa wakuu wa nchi za Kusini watoa wito wa kukomesha mgogoro kati ya Israel na Palestina
Wawakilishi wa ngazi ya juu na wakuu wa Umoja wa Mataifa wakihudhuria Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi za Kusini mjini Kampala, Uganda, Januari 21, 2024. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)
KAMPALA - Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi za Kusini uliowakutanisha pamoja viongozi wa nchi wanachama wa Kundi la 77 na China umemalizika Jumatatu katika mji mkuu wa Uganda, Kampala huku viongozi walioshiriki wakitoa wito wa kusimamishwa mara moja kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza na kulinda raia.
Mkutano huo wa siku mbili, umelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lifanye juhudi za kutekeleza maazimio yake ya kumaliza mgogoro kati ya Israel na Palestina bila kuchelewa.
"Pia tunasisitiza hitaji letu la kuondolewa mara moja na kikamilifu kwa udhibiti wa Israel uliowekwa kwa nguvu kwenye Ukanda wa Gaza, ambao ni sawa na adhabu kubwa ya jumla," viongozi hao wamesema katika nyaraka ya matokeo ya mkutano huo.
Wametoa wito wa kuvunjwa kikamilifu na kusitishwa mara moja shughuli zote haramu za makazi ya Israel katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ikiwemo Jerusalem Mashariki na Eneo la milima ya Golan la Syria linalokaliwa kwa mabavu.
Viongozi hao wamesema kuwa Israel inakiuka Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa kwa kushambulia miundombinu ya kiraia ya Syria, ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege vya kiraia, hali ambayo inatishia maisha ya raia, inazuia operesheni za kibinadamu za Umoja wa Mataifa, na kuhatarisha usalama wa usafiri wa anga.
Aidha wameeleza kuwa Israel inapaswa kukomesha ukiukaji wake wa mamlaka ya Lebanon kwa njia ya anga, nchi kavu na baharini, jambo ambalo linatishia usalama na maendeleo yake ya kiuchumi.
Mkutano wa nchi za Kusini ndiyo chombo kikuu cha kufanya maamuzi cha Kundi la 77 linalojumuisha nchi wanachama 134. Wawakilishi wa ngazi ya juu kutoka nchi karibu 100 na wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa walihudhuria mkutano huo. Mkutano huo wa mwaka huu umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo "Kutoacha Yeyote Nyuma."
Uganda ilichukua uenyekiti wa mkutano huo kutoka kwa Cuba. Hii ni mara ya kwanza kwa Mkutano huo kufanyika barani Afrika. Mikutano miwili ya awali ilifanyika Havana, Cuba, Mwaka 2000, na Doha, Qatar, Mwaka 2005, mtawalia.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda akizungumza kwenye Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi za Kusini mjini Kampala, Uganda, Januari 21, 2024. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma