

Lugha Nyingine
China na Tanzania zaahidi kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya mafanikio makubwa zaidi
DAR ES SALAAM – Naibu Waziri Mkuu wa China Liu Guozhong, ambaye aliongoza ujumbe wa serikali ya China, amefanya ziara nchini Tanzania kuanzia Jumatatu hadi Jumatano. Katika ziara yake hiyo amekutana na Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakibadilishana mawazo ya kina kuhusu uhusiano wa pande mbili na ushirikiano halisi katika nyanja mbalimbali.
Liu, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amewasilisha salamu kutoka kwa Rais Xi Jinping wa China na Waziri Mkuu Li Qiang kwa wenzao wa Tanzania, mtawalia, na kupongeza mafanikio ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania.
Tangu Novemba 2022, wakuu wa nchi hizo mbili wamekutana mara mbili ili kuweka dira ya maendeleo ya uhusiano baina ya nchi hizo mbili, Liu amesema.
Ameeleza kuwa, China inapenda kutumia fursa ya maadhimisho ya kutimia miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, na kufuata uelekezi wa makubaliano ya kimkakati yaliyofikiwa na marais hao wawili, kuimarisha urafiki wa jadi, kuimarisha hali ya kuaminiana kisiasa, kuzidisha mawasiliano na ushirikiano na kuhimiza ujenzi wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Tanzania na kati ya China na Afrika.
Kwa upande wao Rais Samia na Waziri Mkuu Majaliwa wa Tanzania wamemuomba Liu kufikisha salamu zao za dhati kwa wenzao wa China.
Rais Samia amesema kuwa mawasiliano ya karibu ya ngazi ya juu kati ya Tanzania na China yameongeza msukumo mkubwa katika ushirikiano wa kirafiki baina ya nchi hizo mbili.
Amesema, Tanzania daima imekuwa ikifuata kwa uthabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja, ikiichukulia Taiwan kama sehemu isiyoweza kutengwa ya ardhi ya China na kuunga mkono mambo makuu ya China ya kuungana tena.
Amesema Tanzania inapenda kuimarisha muunganiko wa mkakati yake na China na kuimarisha mawasiliano ya vyama na ushirikiano halisi wa pande mbili.
Kwa upande wake Majaliwa amesema tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia miaka 60 iliyopita, ushirikiano kati ya Tanzania na China umezidi kuwa wa karibu, na urafiki wao ni thabiti kama mwamba.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma