Rais Xi atoa wito kwa China na Ufaransa kuanzisha kwa pamoja njia ya amani, kupiga hatua kwa maendeleo ya binadamu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 29, 2024

BEIJING - Kwa kuwa Dunia ya leo kwa mara nyingine iko katika njia panda muhimu, China na Ufaransa zinapaswa kuanzisha kwa pamoja njia ya amani, usalama, ustawi na kupiga hatua kwa maendeleo ya binadamu, Rais wa China Xi Jinping amesema siku ya Jumamosi alipotumiana pongezi na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, katika maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

China na Ufaransa ziliweka pembeni Vita Baridi na kuvuka mgawanyiko kati ya kambi tofauti ili kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia katika ngazi ya kibalozi miaka 60 iliyopita, Rais Xi ameeleza, huku akiongeza kuwa tukio hilo la kihistoria limesukuma uhusiano wa nchi zote duniani uendelee kwa mwelekeo sahihi wa mazungumzo na ushirikiano, ambao bado unatoa ufunuo kwa Dunia ya leo.

Amesema, katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, nchi hizo mbili zimetilia maanani kufanya machaguo ya kimkakati bila ushawishi wa nje, na siku zote zimejitoa kufikia maendeleo kwa pamoja kupitia ushirikiano wa kunufaishana, kuhimiza kufundishana kati ya ustaarabu mbalimbali kupitia mawasiliano kwa usawa, na kukabiliana kwa pamoja na changamoto za kimataifa kwa kupitia uratibu wa pande nyingi.

Huku zikikabiliana na masuala ya nyakati na historia kuhusu wapi Dunia inapaswa kuelekea, China na Ufaransa, zikiwa nchi kubwa zinazojitawala na wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zinapaswa kushikamana na nia ya awali ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kubeba wajibu wao, na kwa pamoja kufungua njia ya amani, usalama, ustawi na kupiga hatua kwa maendeleo ya binadamu, amesema.

Kwa upande wake Macron katika salamu zake za pongezi ameeleza kuwa, kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Ufaransa na China miaka 60 iliyopita ni uamuzi wa kihistoria wa kutupia macho mbali.

Katika kukabiliana na changamoto za kimataifa za hivi sasa, ambazo hazikutokea hapo kabla, ushirikiano kati ya Ufaransa na China, na kati ya Ulaya na China, ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote hapo kabla, ili kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa changamoto za kimataifa, ameongeza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha