Kenya yapokea dola milioni 46 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya upanuzi wa nishati endelevu

(CRI Online) Februari 01, 2024

Mfuko wa uwekezaji katika tabia nchi (CIF), unaosimamiwa na Benki ya Dunia, umetangaza kuongeza dola za Kimarekani milioni 46.39 kwa Kenya ili kuimarisha matumizi ya nishati endelevu nchini humo.

Mkurugenzi mtendaji wa mpito wa mfuko huo Bw. Luis Tineo, amesema kuwa ufadhili huo wa masharti nafuu utasaidia uwekezaji unaolenga kuboresha usambazaji wa umeme na uthabiti wa gridi ya taifa, ili kuiwezesha Kenya kutumia vyanzo zaidi vya nishati ya jua na upepo.

Wizara ya Nishati ya Kenya imesema asilimia karibu 90 ya nishati nchini Kenya inatokana na vyanzo endelevu, huku asilimia 45 ikitokana na joto la ardhi na asilimia 26 kutokana na nishati ya maji. Wizara hiyo imesema, mpango huo utaisaidia Kenya katika azma yake ya kufikia asilimia 100 ya nishati safi katika mfumo wa nishati ifikapo 2030 na kuiweka kwenye njia ya kufikia utoaji sifuri wa hewa chafuzi ifikapo 2050.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha