Muhimbili yatumia saa 6 kutenganisha mapacha

(CRI Online) Februari 02, 2024

Saa sita zimetumika kuwatenganisha watoto mapacha wa kike wenye umri wa miezi 10 wakazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, Tanzania ambao walizaliwa Machi mwaka jana wakiwa wameungana eneo la kifua na tumbo.

Upasuaji huo ni wa kwanza kufanywa na madaktari wazawa nchini Tanzania. Akizungumza Januari 30, 2024, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dk Rachel Mhaville amesema upasuaji huo umefanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kununua vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuwasomesha wataalamu.

Amesema, hata hivyo pamoja na kufanikiwa kufanya upasuaji huo bado wataendelea kushirikiana na wataalamu wengine kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi na kuendeleza uhusiano.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Dk Victor Ngota amesema upasuaji wa kutenganisha watoto unahitaji utaalamu wa hali ya juu hivyo ulihusisha jopo la wataalamu mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa wa upasuaji watoto, upasuaji rekebishi, wataalamu wa usingizi, wataalamu wa lishe pamoja na wataalamu wa radiolojia.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha