Afrika yaomboleza kifo cha Rais Hage Geingob wa Namibia

(CRI Online) Februari 05, 2024

Salamu za rambirambi zinamiminika kutoka nchi mbalimbali za Afrika baada ya Rais wa Namibia Hage Geingob kufariki dunia mapema Jumapili.

Katika salamu zake za rambirambi, Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi amemuelezea Geingob kama rafiki wa kweli wa Botswana. Na kwamba wanathamini sana msaada wake katika kujenga ushirikiano wa pande mbili ambao hivi leo watu wanaufurahia. Masisi ameagiza bendera za Botswana kupepea nusu mlingoti kote nchini kuanzia Jumapili hadi Geingob atakapozikwa.

Naye Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa akiomboleza kifo cha Geingob, amesema Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imepoteza gwiji wa ukombozi na nguli.

Kwa upande wake Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ameelezea masikitiko yake juu ya kifo cha Geingob akisema, Geingob alikuwa mwanajeshi mkongwe wa ukombozi wa Namibia kutoka kwenye ukoloni na ubaguzi wa rangi.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pia ametoa salamu za rambirambi kupitia Mtandao wa X, zamani ikijulikana kama Twitter, akisema amesikitishwa sana kusikia kifo cha Rais wa Namibia, Mheshimiwa Hage Geingob, ambaye ni kaka mpendwa, mwana-Afrika, na rafiki mkubwa wa Tanzania.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha