

Lugha Nyingine
WHO yatoa wito wa kuchukuliwa hatua mahsusi ili kupunguza mzigo wa saratani barani Afrika
Mzigo unaoongezeka wa saratani barani Afrika unapaswa kuchukuliwa kama tahadhari kwa serikali kuchukua hatua mahsusi ambazo zinalenga kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo.
Hayo yamo kwenye taarifa iliyotolewa Jumapili na Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, Matshidiso Moeti, kwenye maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani huko Nairobi nchini Kenya. Amesema bara hilo linakabiliwa na janga la saratani ambalo linaharibu maisha ya watu na kupunguza muda wa kuishi, hivyo kuna ulazima wa kuwekeza katika hatua za kuzuia na kudhibiti ugonjwa huo.
Amebainisha kuwa hali ya saratani barani Afrika inakatisha tamaa. Katika Mwaka 2022, wagonjwa wapya takriban 882,000 wa saratani waligundulika katika kanda ya Afrika ya WHO ikiwa ni pamoja na vifo vya watu karibu 573,000.
Kwa mujibu wa Moeti, asilimia takriban 50 ya saratani mpya zinazogunduliwa miongoni mwa watu wazima barani Afrika ni saratani ya matiti, shingo ya kizazi, tezi dume, utumbo mpana na ini.
Pia amepongeza maendeleo makubwa ambayo nchi za Afrika zinapata katika vita dhidi ya saratani, akibainisha kuwa nchi 17 tayari zimeanzisha vipimo vya juu vya uchunguzi kwa mujibu wa mapendekezo ya WHO.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma