Mkutano wa Madini wa Indaba wa Afrika wafunguliwa mjini Cape Town huku wito wa ushirikiano ukitolewa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 06, 2024

Watu wakihudhuria Mkutano wa 30 wa Uwezekezaji wa Madini Barani Afrika wa Indaba Mwaka 2024 huko Cape Town, Afrika Kusini, Februari 5, 2024. (Xinhua/Wang Lei)

Watu wakihudhuria Mkutano wa 30 wa Uwekezaji wa Madini Barani Afrika wa Indaba Mwaka 2024 huko Cape Town, Afrika Kusini, Februari 5, 2024. (Xinhua/Wang Lei)

CAPE TOWN – Mkutano wa 30 wa Uwekezaji wa Madini wa Indaba Barani Afrika Mwaka 2024 umeanza Jumatatu mjini Cape Town, huku Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akitoa wito wa ushirikiano ili kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo.

Mkutano huo, unaofanyika chini ya kaulimbiu isemayo "Kukumbatia nguvu ya mageuzi chanya: mustakabali mpya wa uchimbaji madini wa Afrika," unatarajiwa kuendelea hadi Alhamisi na kuvutia wajumbe 10,000, wakiwemo mamia ya wadau wa sekta hiyo. Neno "Indaba" linatokana na lugha ya Kizulu, ambayo ina maana ya mkutano wa kujadili mada nzito.

Akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi siku ya Jumatatu, iliyohudhuriwa pia na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema na Waziri Mkuu Sama Lukonde wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pamoja na mawaziri na naibu mawaziri kutoka katika Bara la Afrika, Ramaphosa amesema kuwa uchimbaji madini umekuwa nguzo ya uchumi wa Afrika Kusini kwa karibu miaka 150.

Kwa mujibu wake, sekta ya madini inachangia asilimia 7.5 katika pato la taifa la Afrika Kusini (GDP) na inachangia karibu asilimia 60 ya thamani yote ya mauzo ya nje ya nchi hiyo.

"Sote tunafahamu vema kwamba tunakabiliwa na changamoto kubwa, na changamoto kadhaa endelevu zinakwamisha ufanisi wa uchimbaji madini," Ramaphosa ameonya. "Kimataifa, kuyumba kwa bei za bidhaa, bei ya juu ya nishati, mivutano ya siasa za kijiografia na kuongezeka kwa gharama za maisha duniani vinadhoofisha mazingira ya uendeshaji wa biashara."

Katika majumuishi ya malengo ya serikali, Ramaphosa ameangazia usambazaji thabiti wa umeme, mageuzi ya kiuchumi ya kuboresha mazingira ya uendeshaji wa biashara, vita dhidi ya uchimbaji haramu wa madini na uharibifu wa miundombinu, na uboreshaji wa mazingira ya usimamizi.

Amesisitiza hali ya ushirikiano inayohitaji kusimamiwa na wahusika wote, ikijumuisha viwanda, serikali, na washirika wa kijamii ili kutimiza malengo haya.

Kwa mujibu wa tovuti yake rasmi, Indaba inaelezwa kuwa mkutano mkubwa zaidi wa uwekezaji wa madini duniani, unaojikita katika upatikanaji wa mtaji na maendeleo ya uchimbaji madini barani Afrika.

Watu wakihudhuria Mkutano wa 30 wa Uwezekezaji wa Madini Barani Afrika wa Indaba Mwaka 2024 huko Cape Town, Afrika Kusini, Februari 5, 2024. (Xinhua/Wang Lei)

Watu wakihudhuria Mkutano wa 30 wa Uwekezaji wa Madini Barani Afrika wa Indaba Mwaka 2024 huko Cape Town, Afrika Kusini, Februari 5, 2024. (Xinhua/Wang Lei)

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha