Wachina wanaoishi nchini Tanzania washerehekea Mwaka Mpya wa Jadi wa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 07, 2024

DAR ES SALAAM - Wachina wanaoishi nchini Tanzania wamesherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya ujao wa Jadi wa China, katika tafrija iliyofanyika Jumatatu usiku kwenye ubalozi wa China ulioko mji wa bandari wa Dar es Salaam, ambapo Watanzania waalikwa walijumuika na marafiki zao wa China, wakionyesha urafiki wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Chen Mingjian, Balozi wa China nchini Tanzania, amesema Mwaka Mpya wa Jadi wa China, sikukuu muhimu ya kuunganisha familia, ni shughuli ya kawaida ya Wachina ndani na nje ya nchi na ni sehemu muhimu ya utamaduni wa jadi wa China.

"Inabeba amani, urafiki, maelewano na dhana nyingine za ustaarabu wa China, pamoja na matarajio ya kawaida ya binadamu wote ya kuunganisha, kufurahia, kuridhika na kuwa na ustawi," amesema Chen.

Chen ametoa pongezi kwa Wachina wote wanaoishi nchini Tanzania kwa kuunga mkono kithabiti lengo kuu la kuungana kwa amani kwa nchi mama, kuendeleza ujenzi wa nchi yenye nguvu na ustawishaji mkubwa wa Taifa la China, kukuza maendeleo ya uchumi wa Tanzania, na kutoa mchango mkubwa katika kuhimiza urafiki na ushirikiano wenye matokeo halisi kati ya China na Tanzania.

Naye Kamishna Mkuu wa Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania, Anna Makakala, ameishukuru serikali ya China kwa kuisaidia Tanzania katika kujenga uwezo wa huduma za uhamiaji na kutoa msaada wa kiteknolojia ili kuwezesha huduma za uhamiaji kufikia viwango vinavyotakiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila ametoa shukurani zake kwa jumuiya ya wachina nchini Tanzania kwa mchango wao wa muda mrefu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Mkoa wa Dar es salaam na Tanzania kwa ujumla.

Tafrija hiyo ya mwaka mpya pia yalihudhuriwa na wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali, viongozi waandamizi wa serikali na wanataaluma.

Mwaka Mpya wa Jadi wa China Mwaka 2024 utaangukia tarehe 10 Februari, ikiashiria kuanza kwa Mwaka wa Dragoni.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha