Viongozi wa Afrika wazindua sanamu ya Rais wa zamani wa Tanzania Hayati Nyerere kwenye makao makuu ya AU

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 19, 2024

(Picha inatoka CFP)

(Picha inatoka VCG)

ADDIS ABABA - Viongozi wa Afrika wanaohudhuria Mkutano wa 37 wa Kawaida wa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) Jumapili walizindua sanamu yenye ukubwa wa umbo la Rais wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Nyerere, iliyosimamishwa ndani ya jengo la makao makuu ya chombo hicho cha Afrika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Nyerere ana wasifu wa kuwa mstari wa mbele katika kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ambao ni mtangulizi wa AU ya leo iliyoanzishwa Mwaka 2002. Pia alikuwa mmoja wa waasisi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

"Sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere inatambua mchango wake katika ukombozi, umoja na amani ya Afrika, na inaonyesha fahari yetu katika urithi wetu," Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisema kabla ya hafla ya uzinduzi.

Sanamu ya Nyerere ni sanamu ya tatu kusimamishwa kwenye majengo ya makao makuu ya AU karibu na sanamu za Mfalme wa Ethiopia, Haile Selassie, na Rais wa Ghana hayati, Kwame Nkrumah.

"Hakuna hata mmoja wetu anayeweza kuwa na ustawi wa kudumu bila Afrika yenye ustawi. Ni kweli kusema umaalumu wetu unaendana na hali ya kutegemeana kwetu na kwa hivyo kuendana kwa pamoja kwa ukombozi wa kisiasa na mageuzi ya kiuchumi ni muhimu kwa kuhakikisha mustakabali wetu," Rais Samia amesema.

Waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo ni Rais wa Angola Joao Lourenco, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat.

"Ni furaha kubwa kuwakaribisha katika hafla hii ya uzinduzi wa sanamu ya mmoja wa watu mashuhuri barani Afrika, Mwalimu Julius Nyerere. Urithi wa kiongozi huyu wa ajabu unajumuisha msingi wa mafungamano ya Afrika, busara na kulitumikia bara la Afrika," Faki amesema.

Mwenyekiti huyo wa Kamisheni ya AU amesema Nyerere alitoa mchango anzilishi wa mfano katika kuanzishwa kwa OAU Mwaka 1963, ambalo lilikuwa ni tukio muhimu katika kutafuta umoja wa Afrika.

Sanamu hiyo imebuniwa, kujengwa, na kusafirishwa hadi makao makuu ya AU kwa ushirikiano na SADC, familia ya Nyerere, na serikali ya Tanzania.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha