Mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa asema pingamizi la kusimamisha mapigano Gaza ni sawa na leseni ya kuua

(CRI Online) Februari 21, 2024

(Picha inatoka CRI)

(Picha inatoka CRI)

Kufuatia kura ya turufu ya Marekani dhidi ya rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo inataka kusimamishwa mapigano huko Gaza mara moja, mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Zhang Jun amesema pingamizi la kusitisha mapigano huko Gaza halina tofauti na kuruhusu kuendelea kwa mauaji.

Akitoa ufafanuzi baada ya rasimu ya azimio hilo kupigiwa kura 13 za ndiyo kati ya wanachama 15 wa Baraza la Usalama, ambapo Uingereza ilijizuia, Balozi Zhang, amesema China inaeleza kusikitishwa kwake na kutoridhika na kura ya turufu ya Marekani.

Ameongeza kuwa rasimu ya azimio hilo lililowasilishwa na Algeria kwa niaba ya mataifa ya Kiarabu, kwa kuzingatia mahitaji ya chini ya kibinadamu, linahitajika haraka kutokana na hali iliyopo na linastahili kuungwa mkono na wanachama wote wa Baraza la Usalama.

Hivyo amesema China inaitaka Israel kutii wito wa jumuiya ya kimataifa, kuachana na mipango yake ya kuishambulia Rafah, na kukomesha kuwaadhibu watu wa Palestina.

Amesema China pia inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunganisha juhudi zote za kidiplomasia ili kuwapa watu wa Gaza nafasi ya kuishi, kuwapa watu wa eneo zima la Mashariki ya Kati nafasi ya kuwa na amani, na kutoa fursa ya haki kutendeka.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha