China yaendelea kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika kwa miaka 15 mfululizo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 21, 2024

Katika mkutano maalum na waandishi habari kuhusu Eneo Kielelezo la Ushirikiano wa kina wa Kiuchumi na Kibiashara wa China na Afrika uliofanywa na Wizara ya Biashara ya China hivi karibuni, ilielezwa kwa waandishi wa habari kwamba, China imeendelea kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika kwa miaka 15 mfululizo.

Mnamo mwaka 2023, thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili ilifikia kiwango cha juu katika kihistoria cha Dola za Marekani bilioni 282.1, ikiongezeka kwa 1.5% kuliko mwaka jana.

Mazao ya kilimo yanayoagizwa na China kutoka Afrika yamekuwa sehemu kubwa ya ongezeko hilo la thamani ya biashara. Mwaka 2023 uagizaji wa njugu, mboga za majani, maua na matunda kutoka Afrika kwa China uliongezeka kwa 130%, 32%, 14% na 7% mtawalia. Bidhaa za mashine na za kielektroniki zimekuwa “nguvu kuu” katika bidhaa zinazouzwa na China kwa Afrika. Mauzo ya nje ya China kwa Afrika ya bidhaa za magari yayotumia nishati mbadala, betri za lithium na bidhaa za uzalishaji umeme kwa nishati ya jua yameongezeka kwa 291%, 109% na 57% mtawalia kuliko mwaka jana, zikiunga mkono mageuzi ya nishati mbadala ya Afrika.

Ushirikiano wa China na Afrika katika ujenzi wa miundombinu umepata mafaniko dhahiri. Thamani ya jumla ya mikataba ya ujenzi iliyotiwa saini na kampuni za China kwa upande wa Afrika imefikia zaidi ya bilioni 700.

Ushirikiano katika maeneo yanayoibukia kiuchumi kama vile uchumi wa kidijitali, maendeleo ya kijani na yenye kutoa kaboni chache, usafiri wa anga na wa anga ya juu, huduma za fedha unaendelea kupanuka, ukitia uhai mpya kwa uendelevu katika ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa pande hizo mbili. China na Afrika zimefanikiwa kwa pamoja kufanya “Tamasha la Kununua Bidhaa Bora kutoka Afrika Mtandaoni”, ambalo limehimiza kampuni za China kuchangia kwa hamasa maendeleo ya biashara ya mtandaoni, malipo kwa simu, burudani na sekta nyingine mbalimbali za Afrika. China imetia saini makubaliano ya usafiri wa anga wa kiraia na nchi 27 za Afrika, na imejenga na kurusha satelaiti za mawasiliano ya hali ya hewa za Algeria, Nigeria na nchi nyingine kwa mafanikio.

Hivi karibuni, “Mpango wa jumla wa Ujenzi wa Eneo Kielelezo la Ushirikiano wa kina wa Kiuchumi na Kibiashara wa China na Afrika” umepitishwa na Baraza la Serikali la China na kutolewa rasmi kwa umma, ukiunga mkono mkoa wa Hunan, China katika ujenzi wa eneo hilo.

Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Asia ya Magharibi na Afrika ya Wizara ya Biashara ya China, Jiang Wei amesema, upande wa China utaendelea kushikilia kanuni za udhati, matokeo halisi, urafiki na nia njema, pamoja na muono sahihi wa haki na maslahi, na kufanya kazi na Afrika ili kunufaisha zaidi watu wa China na Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha