

Lugha Nyingine
Wakimbizi karibu 100 wa Burundi waliokuwa Rwanda warejea nyumbani
Wakimbizi takriban 96 wa Burundi, ambao wengi wao walikimbilia Rwanda mwaka 2015 kutokana na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa, wamerejeshwa makwao.
Kiongozi wa kambi ya wakimbizi ya Mahama nchini Rwanda, Andres Vuganeza amesema kuwa kundi hilo linajumuisha watu 78 kutoka Kambi hiyo, na wengine kutoka Kigali, mji mkuu wa Rwanda.
Wakimbizi hao wamekabidhiwa kwa mamlaka za Burundi kwenye mpaka wa Rwanda na Burundi huko Nemba. Ameongeza kuwa wale waliorejeshwa wameamua kurejea Burundi kwa hiari yao.
Burundi ilifunga mpaka wake na Rwanda mwezi Januari, ikiwa ni sehemu ya kulipiza madai ya kwamba Rwanda inaliunga mkono kundi la waasi wa Burundi la Red Tabara, linalolaumiwa kwa mashambulizi ya mwezi Disemba mwaka jana ambapo watu 20 waliuawa kwenye mpaka wa magharibi wa Burundi na DRC.
Hata hivyo Vuganeza amesema kufungwa kwa mpaka huo hakuathiri urejeshwaji huo.
Urejeshaji kwao wa wakimbizi hao umewezeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma