Serikali ya Tanzania kuendeleza umeme wa jotoardhi

(CRI Online) Februari 22, 2024

Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Doto Biteko amesema Serikali ya Tanzania imeamua kwa dhati kuendeleza vyanzo vya umeme wa Jotoardhi ili kuhakikisha Tanzania inazalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya wananchi.

Dk. Biteko amesema hayo mara baada ya kukagua vyanzo vya umeme wa jotoardhi vya Kiejo-Mbaka vyenye kuzalisha umeme wa Megawati 60 na Ngozi chenye uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 70 mkoani Mbeya, na kusema vyanzo hivyo vya umeme vitaongeza nguvu katika vyanzo vilivyopo vya maji na gesi asilia.

Amesema ni lazima miradi ya Jotoardhi ianze, na wataanza na mradi wenye kuzalisha umeme wa megawati 10 katika eneo la Kiejo-Mbaka na Ngozi huku mingine ikifuata.

Amesema hii inajumuisha miradi mingine kama ule wa kuzalisha umeme kwa jua wa eneo la Kishapu wenye uwezo wa umeme wa Megawati 150 ambao umeanza kutekelezwa, mradi wa kuzalisha umeme kwa upepo wa Makambako na mradi wa Malagarasi ambao mkandarasi ameshasaini mkataba tayari kwa kuanza kazi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha