Tanzania kuagiza tani 300,000 za sukari ili kumaliza uhaba uliopo

(CRI Online) Februari 23, 2024

Tanzania inakusudia kuagiza tani zaidi ya 300,000 za sukari mwaka huu ili kumaliza uhaba uliopo wa bidhaa hiyo.

Akiongea na wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Kilimo wa Tanzania Hussein Bashe amesema tani zaidi ya 25,000 za sukari kwa sasa zinashushwa kwenye meli zilizopo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Bashe ameongeza kuwa uagizaji wa sukari tani zaidi ya 300,000 utasimamiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula wa Tanzania (NFRA), akitumai kuwa upatikanaji wa sukari utatengemaa kuanzia mwezi ujao.

Bashe amekemea wauzaji wa sukari kwa kupandisha bei ya bidhaa hiyo, akisema mamlaka imeanzisha msako mkali dhidi ya wafanyabiashara wanaohodhi na kupandisha bei ya sukari kinyume na bei elekezi iliyowekwa na serikali.

Juzi Jumatano, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, aliwaonya wafanyabiashara wanaohodhi sukari, akisema wote wanaohusika na ubadhirifu huo watachukuliwa hatua kali za kisheria. Mchengerwa pia amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuwachukulia hatua kali wanaohodhi bidhaa hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha