Mfalme wa Jordan aonya juu ya kupanuka kwa mgogoro ya Gaza katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 26, 2024

Mfalme Abdullah II wa Jordan (Kati) akikutana na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas (kushoto) mjini Amman, Jordan mnamo Februari 25, 2024. (Kasri la Kifalme la Hashemite/ Xinhua)

Mfalme Abdullah II wa Jordan (Kati) akikutana na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas (kushoto) mjini Amman, Jordan mnamo Februari 25, 2024. (Kasri la Kifalme la Hashemite/ Xinhua)

AMMAN - Mfalme Abdullah II wa Jordan ameonya siku ya Jumapili kwamba kuendelea kwa vita huko Gaza katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kunaweza kuhatarisha kupanuka kwa mgogoro huo.

Mfalme Abdullah ameyasema hayo mjini Amman alipokutana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina, ambapo ametoa wito wa kufanyika juhudi kubwa zaidi ili kufikia usimamishaji vita wa mara moja na wa kudumu huko Gaza, na kulinda raia wasio na hatia, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kasri la Kifalme la Hashemite.

Mfalme huyo amebainisha kuwa Jordan itaendelea kutoa misaada ya kibinadamu, uungaji mkono, na matibabu kwa watu wa Gaza, taarifa hiyo imeongeza.

Amesisitiza Jordan inapinga majaribio yoyote ya kutenganisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza, huku akitaka kuendelea kwa uratibu wa Nchi za Kiarabu kutafuta suluhu ya haki kwa suala la Palestina kwa kuzingatia suluhu ya nchi mbili.

Kwa upande wake Abbas, ametoa pongezi kwa misimamo thabiti ya Jordan kuhusu mgogoro kati ya Kundi la Hamas na Israel akisisitiza haja ya kuendeleza uratibu na mashauriano ya karibu kati ya pande hizo mbili ili kuwezesha harakati ya Wapalestina na kulinda maeneo matakatifu katika mji huo wa Gaza.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha