

Lugha Nyingine
Safari za abiria kwenye reli ya mwendo kasi ya Jakarta-Bandung zafikia milioni 2
Wasanii wa ngoma ya simba wakipiga picha na treni ya mwendo kasi inayotumia njia mbalimbali za nishati ya umeme (EMU) kwenye jukwaa la abiria kupanda na kushuka katika Stesheni ya Reli ya Padalarang ya Reli ya Mwendo kasi ya Jakarta-Bandung huko Padalarang, Indonesia, Februari 10, 2024. (Picha na Septianjar Muharam/Xinhua)
JAKARTA - Reli ya Mwendo Kasi ya Jakarta-Bandung (HSR), ambayo ni ya kwanza ya aina yake nchini Indonesia na Asia Kusini-Mashariki, imesafirisha abiria zaidi ya milioni 2 kwa jumla, limesema Kampuni ya Kimataifa ya Reli ya China siku ya Jumapili.
Kampuni hiyo imesema, reli hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa usalama kwa siku 139, ikibeba abiria jumla ya 2,008,387, tangu ianze kufanya kazi rasmi Oktoba 17, 2023.
Kwa sasa, usafiri wa treni wa kila siku kwenye reli hiyo umeongezwa kutoka mara 14 hadi 40, na idadi ya viti vya abiria imeongezeka mara tatu kutoka 8,400 hadi zaidi ya 24,000. Idadi kubwa zaidi ya abiria waliosafiri kwa siku moja ilikuwa 21,537, wakati kiwango cha juu zaidi cha kila siku cha viti kujaa kikamilifu kilichorekodiwa kilikuwa asilimia 99.6.
Ili kukidhi vizuri zaidi mahitaji ya abiria, sera nyumbulifu ya nauli ilianzishwa, ratiba ya safari za abiria iliboreshwa, na usafiri wa treni uliongezwa siku za likizo, kampuni hiyo imesema.
Ikiwa imesanifiwa kwa kasi ya kilomita 350 kwa saa, reli hiyo yenye urefu wa kilomita 142.3 inafupisha muda wa safari kati ya mji mkuu wa Indonesia, Jakarta hadi Bandung katika Jimbo la Java Magharibi kutoka saa zaidi ya tatu hadi dakika 40 hivi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma