Raia wa Zimbabwe wapiga kambi mbele ya ubalozi wa Marekani wakipinga vikwazo vipya vya Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 08, 2024

Mwanamke akiwa ameshikilia bango kupinga vikwazo vya Marekani mbele ya Ubalozi wa Marekani mjini Harare, Zimbabwe, Machi 5, 2024. (Picha na Tafara Mugwara/Xinhua)

Mwanamke akiwa ameshikilia bango kupinga vikwazo vya Marekani mbele ya Ubalozi wa Marekani mjini Harare, Zimbabwe, Machi 5, 2024. (Picha na Tafara Mugwara/Xinhua)

HARARE - Kundi la kupinga vikwazo lililopiga kambi mbele ya Ubalozi wa Marekani mjini Harare kupinga vikwazo vya Marekani dhidi ya Zimbabwe limeapa kuwa ni hadi vikwazo vyote vitakapoondolewa ndipo kambi hiyo itavunjwa.

"Tumepiga kambi nje ya Ubalozi wa Marekani kwa karibu miaka mitano sasa, na tutaendelea kupiga kambi hapa hadi vikwazo vyote vitakapoondolewa bila masharti," Sally Ngoni, msemaji wa Muungano Mpana Dhidi ya Vikwazo, ambao umekuwa ukipiga kambi tangu Machi 2019, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua siku ya Jumanne.

Kambi hiyo iliyowekwa moja kwa moja mbele ya ubalozi inaashiria hali mbaya ya maisha ya watu wa Zimbabwe iliyosababishwa na vikwazo hivyo vilivyodumu kwa miongo zaidi ya miwili, amesema.

Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumatatu alitia saini amri ya kusitisha mpango wa vikwazo dhidi ya Zimbabwe ambao umekuwa ukitekelezwa tangu Mwaka 2003, lakini wakati huo huo akaweka vikwazo dhidi ya watu 11 wa Zimbabwe, akiwemo Rais Emmerson Mnangagwa, na vyombo vitatu, kwa madai ya kuhusika katika rushwa au ukiukaji wa haki za binadamu chini ya Sheria ya Uwajibikaji ya Haki za Kibinadamu ya Marekani ya Magnitsky.

“Tunaona ni hatua kubwa kwamba wameondoa amri hizo za vikwazo, ingawa tunahisi pia ni kama wametupiga kofi usoni kwa sababu wameongeza vyombo na watu wengine kwenye orodha ya vikwazo,” amesema Ngoni.

Mwaka jana, kundi hilo liliwasilisha ombi kwenye Mahakama Kuu mjini Harare, likitaka Marekani ilipe fidia kwa kuweka vikwazo hivyo.

Akiongea na wanahabari siku ya Jumatano, Kaimu Balozi wa Marekani mjini Harare Laurence Socha alisema vikwazo hivyo vinalenga tu "watu na vyombo mahususi na wazi."

Rutendo Matinyarare, mwenyekiti wa Vuguvugu la Kupinga Vikwazo la Zimbabwe, kundi ambalo limepeleka mapambano dhidi ya vikwazo kwenye mahakama za kimataifa, ameliambia Xinhua Jumatano kwamba vikwazo hivyo ni kinyume cha sheria.

Katika taarifa yake Jumatano usiku, serikali ya Zimbabwe ililaani hatua ya Marekani ya kuondoa vikwazo hivyo kwa kiwango kidogo na kutaka kuondolewa kabisa.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Deng Jie)

Picha