

Lugha Nyingine
Idadi ya watalii waliotembelea mbuga za wanyama za Tanzania yaongezeka
Msemaji wa Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ya Tanzania Bw. Mobhare Matinyi amesema idadi ya watalii wanaotembelea mbuga 22 za taifa za Tanzania iliendelea kuongezeka katika mwaka uliopita licha ya uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika mbuga nyingi za taifa.
Bw. Matinyi amesema kati ya Julai 2023 na Februari 2024 watalii zaidi ya milioni 1.45 walitembelea Mbuga za Taifa za Tanzania, huku mbuga ya Taifa ya Serengeti ikiwa kivutio kikuu.
Shirika la Hifadhi za Taifa la Tanzania (TANAPA) liweka lengo la kuvutia watalii zaidi ya milioni 1.37 kati ya mwaka 2023 hadi 2024. Hata hivyo takwimu za hivi punde zinaonyesha kuwa lengo hilo limevukwa.
Mvua kubwa iliyonyesha na kuathiri miundombinu katika hifadhi nyingi za Taifa nchini humo, haikuzuia watalii, ameongeza msemaji huyo huku akibainisha kuwa TANAPA inaendelea na kazi ya kukarabati barabara zilizoharibika ili kuhakikisha mtiririko mzuri wa watalii.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma