Rais wa Rwanda akubali kukutana na mwenzake Tshisekedi kuhusu mgogoro wa mashariki mwa DRC

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 12, 2024

LUANDA - Rais wa Rwanda Paul Kagame amekubali kukutana na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi kujadili mgogoro unaoendelea mashariki mwa DRC, huku tarehe na sehemu ya kukutana bado havijaamuliwa.

Utayari wa mazungumzo umedhihirika kwenye ziara ya Rais Kagame mjini Luanda, mji mkuu wa Angola, siku ya Jumatatu, ambapo alikutana na Rais wa Angola Joao Lourenco. Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola Tete Antonio ametangaza maendeleo hayo baada ya mkutano kati ya viongozi hao wawili.

Kwa mujibu wa Antonio, Rwanda na DRC zimekubaliana na kanuni ya kufanya mkutano huo, huku ujumbe wa mawaziri kutoka pande zote mbili ukifanyia kazi lengo hilo.

Ziara ya Kagame nchini Angola inafuatia ziara ya Tshisekedi mwishoni mwa Februari, ambapo ilitangazwa kuwa Tshisekedi amekubali kukutana na mwenzake wa Rwanda.

Rais Lourenco, akiwa mpatanishi aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika, amekuwa akiwezesha mkutano kati ya viongozi hao wawili, ingawa tarehe mahususi bado hazijatajwa.

Juhudi za upatanishi zinatokana na haja ya kushughulikia migogoro inayoongezeka hivi karibuni mashariki mwa DRC, hasa inayohusisha kundi la M23, na kurejesha uhusiano kati ya DRC na Rwanda.

DRC imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, tuhuma ambayo imekanushwa na Rwanda na waasi wa M23. Kundi hilo la waasi limezusha migogoro na majanga ya kibinadamu na kuteka ngome kubwa katika ardhi ya DRC. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha