China yazitaka pande husika kufanya juhudi za kusimamisha mapigano katika ukanda wa Gaza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 13, 2024

UMOJA WA MATAIFA - Geng Shuang, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa ametoa wito siku ya Jumatatu wa kuitaka jumuiya ya kimtaifa kufanya juhudi za kusimamisha mapigano mara moja huko Gaza akisema mgogoro wa sasa katika Ukanda wa Gaza umekuwa ukiendelea kwa miezi mitano, ambao umesababisha madhara makubwa kwa wanawake.

Amesema akina mama na mabinti zaidi ya 9,000 wameuawa, na mamia ya maelfu ya wanawake wamekimbia makazi yao.

Jumatatu ni mwanzo wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na China inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na kuongeza juhudi za kuhimiza kusimamisha mapigano mara moja ili kuwawezesha watu wa Gaza bado kuwa na matumaini ya kuishi, Geng amesema kwenye mkutano wa kutoa habari wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu unyanyasaji wa kingono unaohusika na migogoro.

“Pia tunatoa wito wa kuongeza juhudi za kidiplomasia ili mateka wote waachiliwe mapema iwezekanavyo na kujumuika tena na familia zao,” amesema.

Mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu unyanyasaji wa kingono unaohusika na migogoro, Pramila Patten, hivi karibuni aliongoza ujumbe kufanya ziara nchini Israel, ambapo pia ulifanya ziara katika kando za magharibi za Mto Jordan zinazokaliwa.

Ripoti ya ujumbe huo inasema kwamba kuna sababu za kuaminika kwamba unyanyasaji wa kingono unaohusika na migogoro ulitokea katika maeneo kadhaa pembezoni mwa Gaza wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7.

Kuhusiana na mateka, ripoti hiyo imepata taarifa wazi na zenye ushahidi wa kutosha kwamba baadhi yao wamefanyiwa aina mbalimbali za unyanyasaji wa kingono unaohusika na migogoro.

Wakati huo huo, ripoti hiyo imebaini kwamba wanaume na wanawake wa Palestina waliozuiliwa katika kando za magharibi za Mto Jordan zinazokaliwa walitendewa kiukatili, kiunyama na kudhalilishwa vibaya, hivyo hali ya huko imezidi kuwa na utatanishi zaidi. Ripoti hiyo pia imetoa mapendekezo halisi juu ya hatua za kufuata. China inatumai kuwa pande husika zitazipa umuhimu na kufanya juhudi za kuziitikia hatua hizo, amesema.

Amesema China inalaani aina zote za unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake katika migogoro ya silaha, na inatetea kufanya uchunguzi kwa wakati na kwa kina, kuwajibishwa kwa wahalifu, na kutetea haki na utu kwa waathiriwa. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha