Ripoti ya Umoja wa Mataifa yaonya maendeleo yasiyo na uwiano zinaacha maskini zaidi nyuma, na kuzidisha ukosefu wa usawa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 15, 2024

Msimamizi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa Achim Steiner akiongea na waandishi wa habari kuhusu Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya Mwaka 2023/24 (HDR) kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Machi 13, 2024. (Manuel Elias/Picha ya UN/Kupitia Xinhua)

Msimamizi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa Achim Steiner akiongea na waandishi wa habari kuhusu Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya Mwaka 2023/24 (HDR) kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Machi 13, 2024. (Manuel Elias/Picha ya UN/Kupitia Xinhua)

UMOJA WA MATAIFA – Mchakato wa maendeleo yasiyo na uwiano unawaacha maskini zaidi nyuma, na kuzidisha hali ya ukosefu wa usawa, na kuchochea mgawanyiko wa kisiasa kote duniani, kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya Mwaka 2023/24 (HDR) iliyotolewa Jumatano na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) yenye kichwa kisemacho "Kuvunja Mkwamo: Kupanga upya ushirikiano katika Dunia yenye ncha."

Matokeo yake ni "mkwamo hatari" ambao lazima ushughulikiwe haraka kupitia hatua za pamoja, inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inabainisha hali ngumu: kurudi nyuma kwa kasi katika Fahirisi ya Maendeleo ya Binadamu duniani (HDI) – ambacho ni kipimo cha majumuisho yanayoakisi Pato la Taifa la nchi kwa kila mtu, elimu, na umri wa kuishi - vimekuwa kwa sehemu, visivyo kamilifu, na visivyo na usawa.

HDI inakadiriwa kufikia viwango vya juu zaidi Mwaka 2023 baada ya kushuka kwa kasi Mwaka 2020 na 2021. Lakini maendeleo haya hayana usawa. Nchi tajiri zinashuhudia viwango vya juu vya maendeleo ya binadamu wakati nusu ya nchi maskini zaidi duniani zikiendelea kuwa chini ya viwango vyao vya maendeleo vya kabla ya mgogoro.

Hali ya ukosefu wa usawa wa kimataifa inazidi kuwa mbaya zaidi kutokana na mkusanyiko mkubwa wa kiuchumi. Kama ilivyorejelewa katika ripoti hiyo, karibu asilimia 40 ya biashara ya kimataifa ya bidhaa imejikita katika nchi tatu au chache zaidi; na Mwaka 2021 thamani ya mtaji kwenye soko la hisa wa kila moja ya kampuni tatu kubwa zaidi za teknolojia duniani ulizidi pato la taifa (GDP) la asilimia zaidi ya 90 ya nchi duniani mwaka huo.

"Ongezeko la pengo la maendeleo ya binadamu lililobainishwa na ripoti hiyo linaonyesha kuwa mwelekeo wa miongo miwili wa kupunguza kwa kasi hali ya kukosekana kwa usawa kati ya nchi tajiri na maskini sasa unarudi nyuma. Licha ya jamii zetu za kimataifa zilizounganishwa sana, tunashindwa kupunguza hilo. Ni lazima tutumie kikamilifu uhusiano wetu wa kutegemeana na vile vile uwezo wetu wa kushughulikia changamoto zetu za pamoja zinazotishia uwepo wetu na kuhakikisha matarajio ya watu yanafikiwa," amesema Achim Steiner kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasisitiza jinsi kutegemeana kimataifa kunavyojijenga upya na kutoa wito kwa kizazi kipya cha bidhaa za umma duniani.

Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ni uchapishaji huru wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha