Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar watangazwa kuwa moja ya viwanja bora zaidi barani Afrika

(CRI Online) Machi 15, 2024

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume mjini Zanzibar, Tanzania umeshinda tuzo ya kuwa moja ya viwanja vya ndege bora zaidi barani Afrika kupitia kipengele cha Ubora wa Huduma za Viwanja vya Ndege katika tuzo zilizotolewa na Baraza la Viwanja vya Ndege la Kimataifa.

Akiongea na wanahabari Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar Seif Abdalla Juma amesema tuzo hiyo itaongeza ujio wa watalii kutoka nje ya nchi katika Visiwa vya Zanzibar.

Amesema tuzo hiyo inatambua ubora wa uwanja wa ndege kulingana na maoni ya abiria yaliyokusanywa kupitia tafiti za kila siku katika maeneo ya kuondoka na kuwasili duniani kote.

Juma amesema mafanikio hayo yametokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ndiyo uwanja wa ndege pekee Zanzibar. Kampuni ya Uhandisi wa Ujenzi ya Beijing, inayoongoza nchini China, ilijenga kituo cha tatu cha uwanja huo wa ndege.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha