China yapinga Marekani kuzuia haki halali ya maendeleo kwa kisingizio cha ushindani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 19, 2024

BEIJING - China inapinga Marekani kuingilia mambo ya ndani ya China kwa kisingizio cha haki za binadamu na mtazamo wa maadili, na kuzuia haki halali ya maendeleo ya China kwa kisingizio cha ushindani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian amesema Jumatatu.

Msemaji huyo amesema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati akijibu swali kuhusu maoni ya hivi majuzi ya Balozi wa Marekani nchini China Nicholas Burns kuhusu China.

"Tumeona kuwa Balozi Burns hivi karibuni amekuwa akitoa maoni hasi dhidi ya China mara kadhaa. Kauli hizi zinakinzana na makubaliano muhimu ya pamoja waliyofikia marais wa China na Marekani kwenye mkutano wa kilele huko San Francisco," Msemaji amesema, huku akiongeza kuwa maoni hasi kama hayo hayasaidii maendeleo mazuri na ya utulivu ya uhusiano kati ya China na Marekani.

Msemaji huyo amesema China daima inafuata kanuni za kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na kufanya ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote katika kushughulikia na kukuza uhusiano wa pande mbili.

"Tunatumai kuwa Marekani itafanya juhudi pamoja na China kwa mwelekeo sawa katika kutekeleza makubaliano na matarajio muhimu ya pamoja waliyofikia marais wa nchi mbili kwenye mkutano wa kilele huko San Francisco ili kuhimiza maendeleo ya utulivu, mazuri na endelevu ya uhusiano wa pande mbili."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha