China yatoa wito kwa pande zote mbili kwenye mgogoro wa Sudan kusimamisha vita wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani

(CRI Online) Machi 21, 2024

Naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, Balozi Dai Bing amezitaka pande zote mbili kwenye mgogoro wa Sudan kutekeleza matakwa ya azimio namba 2724 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kufikia makubaliano ya kusimamisha vita wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani haraka iwezekanavyo, kuepusha vifo vya raia, na kuzuia kuenea zaidi kwa mgogoro huo katika nchi jirani.

Akizungumza siku ya Jumatano katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la chakula nchini Sudan, Balozi Dai amesema mgogoro wa Sudan unaendelea kuongezeka huku hali ya kibinadamu ikiendelea kuzorota, ambapo watu milioni 18 wanakabiliwa na njaa, na matatizo ya usalama wa chakula ni makubwa katika maeneo mengi.

Amesema China inathamini kazi ya mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, inakaribisha mamlaka ya Sudan kufungua vituo vingi vya kibinadamu na kushirikiana kikamilifu kutoa misaada ya kibinadamu, na kutoa wito kwa pande zote nchini Sudan kuendelea kuhakikisha ufikiaji wa haraka, salama na usio na vikwazo wa huduma za kibinadamu.

Bw. Dai pia amesema, jumuiya ya kimataifa, hasa mashirika ya ufadhili yanapaswa kuwajibika, kuongeza msaada wa kifedha na chakula, kujaribu kupunguza athari za migogoro katika maisha ya watu, na kuepuka maafa makubwa zaidi ya kibinadamu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha