Wawakilishi karibu 2,000 watahudhuria mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia 2024

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 26, 2024

Li Baodong, Katibu Mkuu wa Baraza la Boao la Asia (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa kituo cha waandishi wa habari cha mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia katika Kisiwa cha Boao, Haikou, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Machi 26, 2024 (People’s Daily Online)

Li Baodong, Katibu Mkuu wa Baraza la Boao la Asia (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa kituo cha waandishi wa habari cha mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia katika Boao, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Machi 26, 2024. (Picha na Aris/People's Daily Online)

Baraza la Boao la Asia limefanya mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Machi 26 likielezea kuhusu maandalizi na uratibu wa mkutano wake mkuu wa Mwaka 2024 utakaofanyika Machi 26-29 hapa Boao, Mkoa wa Hainan, China.

Akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, Li Baodong, Katibu Mkuu wa Baraza la Boao la Asia, amewakaribisha wawakilishi karibu 2,000 kutoka nchi na kanda zaidi ya 60 na waandishi wa habari zaidi ya 1,100 kutoka nchi na kanda takriban 40 kuhudhuria mkutano huo wa mwaka.

Li Baodong ametambulisha kuwa kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni "Asia na Dunia: Changamoto za Pamoja na Kuchangia Wajibu" ambayo imetokana na uhalisia kwamba kwa sasa, matatizo yanayoikabili Dunia ni magumu yanahitaji mshikamano na ushirikiano kuyatatua.

“Ni pale tu Jumuiya ya Kimataifa inapokutana na changamoto kwa pamoja, kubeba wajibu kwa pamoja, na kuimarisha ushirikiano ipasavyo ndipo Dunia itaendelea katika njia ya amani na ustawi” amesema Li.

Amesema mkutano wa mwaka huu umepanga mada "4+1", ambazo ni "Uchumi wa Dunia", "Uvumbuzi wa Sayansi na Teknolojia", "Maendeleo ya Jamii", "Ushirikiano wa Kimataifa" na "Kukabiliana pamoja na changamoto".

“Mada nne za kwanza zilizotajwa hapo juu zinazingatia nyanja tofauti, zinachambua kwa kina changamoto na fursa za sasa zinazoikabili Asia na Dunia, na kutafuta fursa za maslahi ya pamoja an kuchangia wajibu katika maendeleo ya Dunia” amesema Li huku akiongeza kuwa, mada ya tano itajadili jinsi ya kuimarisha ushirikiano na kukabiliana na changamoto kwa mtazamo wa wageni mbalimbali watakaohudhuria na kushiriki kwenye mada husika.

Amesema kuwa, inatarajiwa kwamba kupitia mjadala wa mada hizo tano tajwa hapo juu, kutakuwa na kuongezeka zaidi kwa maafikiano kwamba kufikia maendeleo endelevu ni maslahi ya pamoja ya nchi zote duniani, na mshikamano na ushirikiano ni wajibu wa pamoja wa jumuiya ya kimataifa.

Li amesisitiza kuwa kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Dunia kwa sasa ni dhaifu, hali ya kimataifa ni ya machafuko, majanga ya asili na hali mbaya za hewa zimekuwa ni za mara kwa mara huku mahitaji ya usimamizi wa kimataifa yanazidi kuwa ya dharura, na maendeleo na usalama wa dunia unakabiliwa na changamoto nyingi.

Hata hivyo, ameeleza matumaini kwamba, uchumi wa Dunia unatoka hatua kwa hatua kutoka kwenye ukungu wa janga la UVIKO-19, na uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia umeleta kasi mpya ya ukuaji wa uchumi.

Amesema Baraza la Boao linatumai kwamba kupitia mijadala ya mkutano huu wa mwaka, kutakuwa na kukusanywa kwa hekima kutoka pande zote, kuunganisha nguvu ya Asia na Dunia, na kufanya kazi pamoja ili kuondokana na matatizo na kujenga mustakabali wa siku za baadaye pamoja.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha