Ripoti mbili muhimu za Baraza la Boao 2024 zaonesha Asia kuendelea kuwa injini ya ukuaji wa uchumi, nishati safi duniani huku China ikiongoza njia

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 27, 2024

C:\Users\hp\Desktop\1.jpg

Li Baodong, Katibu Mkuu wa Baraza la Boao la Asia (Kulia) akionesha ripoti za mwaka za hali ya uchumi na maendeleo endelevu ya Asia kwa waandishi wa habari kwenye ukumbi wa kituo cha waandishi wa habari cha mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia 2024 hapa Boao, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Machi 26, 2024 (People's Daily Online)

Ripoti mbili za hali ya uchumi na maendeleo endelevu ya Asia kwa mwaka 2024 zilizozinduliwa jana Jumanne, Machi 26 kwenye mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia 2024 unaoendelea zinaonesha kuwa Bara la Asia litaendelea kuwa injini ya ukuaji wa uchumi na nishati safi duniani mwaka 2024 huku China ikiongoza njia.

Ripoti hizo ambazo ni "Ripoti ya mwaka ya mtazamo wa Uchumi na Maendeleo ya Mafungamano ya Asia" na "Baraza la Boao kwa Maendeleo Endelevu ya Asia: Ripoti ya Mwaka ya Asia na Dunia" zimezinduliwa na kutambulishwa kwa umma na Katibu Mkuu wa baraza hilo, Li Baodong.

Ripoti ya mtazamo wa Uchumi wa Asia inaonesha kuwa uchumi wa kimataifa utaendelea kukumbwa na hali ya kutokuwa na uhakika na mifarakano Mwaka 2024, huku uchumi wa Asia kwa ujumla wake bado unakabiliwa na mazingira magumu pamoja na haja ya kukabiliana na changamoto za ndani.

Hata hivyo, kasi ya ukuaji wa uchumi wa Asia na mafungamano ya kiuchumi ya kikanda yataendelea kuwa imara. Ufanisi mzuri wa uchumi wenye matumaini kwa ujumla uko mbioni kufikiwa, sehemu ya ripoti hiyo inasomeka.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa, uchumi wa Asia unatarajiwa kudumisha kiwango cha juu cha ukuaji, ukiwakilisha au kuchukua asilimia 49% ya Pato la jumla la kiuchumi la Dunia Mwaka 2024.

“Licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi za nje, uchumi wa Asia bado utaendelea kudumisha kiwango cha juu cha ukuaji. Huku ukiungwa mkono na matumizi thabiti katika manunuzi na sera zenye matokeo halisi za fedha, kiwango cha ukuaji kinatarajiwa kuvuka kile cha 2023, kikifikia karibu 4.5%, hivyo kuendelea kuwa mchangiaji mkubwa zaidi wa ukuaji wa uchumi duniani” ripoti hiyo inasomeka.

Ripoti hiyo imeangazia masuala mbalimbali kama vile ajira, kipato cha watu, bei za wanunuzi na mfumko wa bei, shughuli za utalii, biashara na uwekezaji, mafungamano ya kiuchumi ya kikanda miongoni mwa mengine mengi.

Kwa upande wa Baraza la Boao kwa Maendeleo Endelevu ya Asia: Ripoti ya Mwaka ya Asia na Dunia, ripoti hiyo imeangazia nguvu ya kifursa ya bara hilo katika kuhamia kwenda nishati mbadala huku China ikiongoza nchi za Asia katika kufanya uwezekezaji mkubwa kwenye eneo hilo.

Ripoti hiyo inasema, China inachangia zaidi ya 50% ya uwezo wa uzalishaji wa umeme barani Asia na karibu 70% ya uwezo wa kuzalisha nishati safi barani Asia. Huku kuanzia Mwaka 2013 hadi 2022, uwezo wa uzalishaji umeme wa China ukiwa ulikua kwa kasi sana.

Aidha, ripoti hiyo inaonesha kuwa uwezo wa kuzalisha umeme barani Asia unaendelea kuongezeka kwa kasi, uwekezaji wa nishati mbadala umeongezeka, na nishati ya jua na upepo ni maeneo muhimu ya maendeleo ya nishati mbadala katika Asia.

C:\Users\hp\Desktop\2.jpg

Waandishi wa habari wakifuatilia utoaji wa ripoti za mwaka za hali ya uchumi na maendeleo endelevu ya Asia kwenye ukumbi wa kituo cha waandishi wa habari cha mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia Mwaka 2024 hapa Boao, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Machi 26, 2024 (People’s Daily Online)

C:\Users\hp\Desktop\4..jpg

Ripoti za mwaka za hali ya uchumi na maendeleo endelevu ya Asia zikionekana katika picha kwenye ukumbi wa kituo cha waandishi wa habari cha mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia Mwaka 2024 hapa Boao, Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Machi 26, 2024 (People’s Daily Online)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha