Mkurugenzi Ali Mchumo aeleza alivyoshuhudia mageuzi makubwa ya China, atoa wito kwa nchi zinazoendelea kuiga mfano

By Aris (Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 27, 2024

Ali Mchumo akihojiwa na People’s Daily Online.

Ali Mchumo akihojiwa na People’s Daily Online. (Picha na Song Ge/People's Daily Online)

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mianzi Duniani (INBAR) Ali Mchumo, ambaye alikuwa Ofisa Mwandamizi wa zamani wa Serikali ya Tanzania, amesema China imepiga hatua kubwa ya mageuzi ya kiuchumi na kupata maendeleo katika muda mfupi uliopita na kwamba nchi zinazoendelea hususan za Afrika zinatakiwa kujifunza kutoka kwa China katika mambo mengi.

Akizungumza hivi karibuni kwenye mahojiano maalum na People’s Daily Online yaliyofanyika ofisini kwake mjini Beijing, China, Mkurugenzi Mchumo amesema yeye binafsi amekuwa akifuatilia maendeleo ya China tangu alipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania hivyo amekuwa na hamu sana ya kuja China kujionea hali ilivyo.

Amesema Mwaka 1978 alipokuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, alibahatika kuja China. “Niliona China ilikuwa ni nchi yenye pilika nyingi, na Beijing ya kipindi hicho ilikuwa imejaa baiskeli nyingi zaidi huku mji ukiwa na uchafuzi mkubwa wa hewa” amesema.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu Mchumo amesema aliporudi tena mwaka 1988, miaka 10 baadaye wakati alipopita Beijing kwenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan, alishuhudia mabadiliko makubwa sana nchini China.

“Haikuwa tena China ile niliyoiona Mwaka 1978, hali ya mitaa na hali ya watu ilikuwa imebadilika sana” amesema Mkurugenzi Mkuu Mchumo huku akiongeza kusema katika miaka yote amekuwa akifuatilia maendeleo makubwa ya hali za watu kutokana na mafanikio ya kuondoa umaskini, ukuaji wa viwanda na hatua kubwa katika uvumbuzi wa teknolojia, mafanikio ya TEHAMA, na watu wanaofuata nidhamu kwenye jamii, na kufuata sheria na utaratibu.

Amesema, moja ya maeneo ambayo China imefanya vizuri ni katika ulinzi na uhifadhi wa mazingira na shirika lake la mianzi limekuwa likishirikiana na China katika kutumia mianzi kama nyenzo ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi duniani kwa njia mbalimbali zikiwemo zile za kuifanya mianzi kuwa mbadala wa plastiki na kuwa kingo za ulinzi wa mito na chanzo cha rutuba ya kilimo.

Wazo la kujenga “China ya Kupendeza” limeisaidia sana China kuwa na mazingira safi, maendeleo yamekuwa ya kijani yanayopunguza uchafuzi kwa mazingira lakini pia imepiga hatua kubwa duniani katika kupunguza utoaji wa hewa ya kaboni huku mito na maziwa yake yakiwa yenye maji safi na yenye kuvutia, amesema Mkurugenzi Mkuu Mchumo.

“Ni mambo ambayo nadhani nchi nyingine zinaweza kujifunza na kuiga” amesema Mkurugenzi Mchumo.

Mwaka huu ni wa maadhimisho ya miaka 60 tangu Tanzania na China zianzishe uhusiano wa kidiplomasia, Mkurugenzi Mkuu Mchumo amesema, katika miaka ya mwanzo kabisa, wakati ndiyo ulipoanzishwa kwa mradi wa reli ya TAZARA ya kuunganisha Tanzania na Zambia, reli hiyo ambayo ilijengwa kwa msaada wa China.

"Mradi huu ambao ulikuwa na umuhimu mkubwa sana kwa ukombozi na kujenga uhusiano kati ya Tanzania na Zambia na China. Mradi huu bado tunaukumbuka na bado unatoa mchango mkubwa sana katika kujenga uchumi wa nchi hizi mbili na kujenga kumbukumbu ya uhusiano kati ya Tanzania na China" amesema.

Ameeleza kuwa katika miaka yote 60 ya uhusiano, ushirikiano wa China na Tanzania katika sekta za afya, elimu, biashara, na mawasiliano kati ya watu yamepata mafanikio makubwa.

Amesema miradi inayojengwa chini ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja imekuwa muhimu sana katika kuunganisha miundombinu si nchi ya Tanzania pekee bali pia kwa bara zima la Afrika

“Nina matumaini makubwa kwamba uhusiano na urafiki huu utazidi kuendelea na utazidi kuleta manufaa makubwa sana kwa nchi yetu lakini pia kwa nchi ya China” amesema Mchumo.

Mkurugenzi Mchumo pia amesema kuwa, China ina maono ya kujenga ushirikiano wa kimataifa kupitia mapendekezo mbalimbali kama vile Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia pamoja na majukwaa ya kukutanisha kwa pamoja viongozi wa China na Afrika.

Amesema miradi na majukwaa haya ya ushirikiano inawezesha kuifanya China ikumbukwe na kupendwa si nchini Tanzania pekee bali Afrika nzima.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha