Israel yaandaa mashambulizi dhidi ya Rafah huku mazungumzo ya kusimamisha mapigano yakianza tena nchini Misri

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 01, 2024

Manusura akiokolewa kutoka kwenye vifusi baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga katika mji wa Rafah, Ukanda wa Gaza, Machi 27, 2024. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

Manusura akiokolewa kutoka kwenye vifusi baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga katika mji wa Rafah, Ukanda wa Gaza, Machi 27, 2024. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

JERUSALEM - Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza Jumapili kwamba jeshi la Israel linajiandaa kushambulia mji wa Rafah, huku mazungumzo ya kusimamisha mapigano yakianza tena nchini Misri.

Rafah, mji wa kusini kabisa wa Gaza, umekuwa kimbilio la Wapalestina zaidi ya milioni moja waliolazimika kukimbia makazi yao wanaotafuta hifadhi kutokana na mashambulizi ya mabomu. Wataalamu wa Umoja wa Mataifa na nchi kadhaa zimeonya kwamba operesheni yoyote ya ardhini katika mji huo itasababisha maafa makubwa kwa raia.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, Netanyahu amesema kufuatia kuidhinisha kwake mpango wa jeshi wa mashambulizi ya ardhini huko Rafah mapema mwezi Machi, jeshi sasa linajitayarisha kuhamisha watu kabla ya kushambulia mji huo.

"Itachukua muda, lakini itafanyika," amesema. "Tutaingia Rafah na kuua vikosi vya Hamas huko. Hakuna ushindi pasipo kuingia Rafah na kuangamiza vikosi vya Hamas huko."

Watu wakisubiri kupokea msaada wa chakula katika Mji wa Rafah, Kusini mwa Ukanda wa Gaza, Machi 30, 2024. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

Watu wakisubiri kupokea msaada wa chakula katika Mji wa Rafah, Kusini mwa Ukanda wa Gaza, Machi 30, 2024. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

Kaskazini mwa Gaza, ambako Umoja wa Mataifa ulisema njaa kali inakaribia, vikosi vya Israel vimeendelea na uvamizi katika Hospitali ya Al-Shifa, ambayo ilikuwa ni kituo kikubwa zaidi cha matibabu kabla ya mgogoro huo wa sasa kuanza.

Kwa mujibu wa Netanyahu, wanamgambo wasiopungua 200 wameuawa katika jengo hilo la matibabu. Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas imesema, makumi ya watu wameuawa katika hospitali hiyo, ambapo wagonjwa na wakimbizi takriban 3,000 walikuwa wakitafuta makazi.

Alasiri siku hiyo ya Jumapili, ujumbe wa Israel wa maafisa wa usalama uliondoka kwa ajili ya kufanya duru mpya ya mazungumzo na wapatanishi mjini Cairo.

Kwa ujumla, Wapalestina wasiopungua 32,782 wameuawa na 75,298 kujeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake ya kulipiza kisasi dhidi ya Kundi la Hamas Oktoba 7, 2023. Idadi ya waliouawa kwa upande wa Israel kutokana na mashambulizi ya kushtukiza ya Hamas imefikia 1,139, huku takriban 100 wakiwa bado wameshikiliwa mateka huko Gaza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha