Ufadhili mpya wa Benki ya Dunia kuboresha reli ya Tanzania

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 01, 2024

DAR ES SALAAM - Reli ya zamani ya kati ya Dar es Salaam na Isaka nchini Tanzania inatarajiwa kufanyiwa maboresho makubwa kufuatia ufadhili mpya ulioidhinishwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA), ambayo ni taasisi ya fedha ya Kundi la Benki ya Dunia, benki hiyo ya kimataifa ya mikopo imesema Ijumaa.

Benki ya Dunia imesema katika taarifa yake kwamba dola za Kimarekani milioni 200 katika kufadhili awamu ya pili ya Mradi wa Maendeleo ya Muunganisho wa Barabara na Reli Tanzania zitaboresha usalama, kuhimili tabianchi na ufanisi wa uendeshaji katika sehemu hiyo ya reli.

Mbali na uimarishaji wa miundombinu na kusaidia tafiti za usafiri, vipengele vya ufadhili huo pia vimejikita katika kuimarisha uhimilivu wa tabianchi wa sehemu ya reli ya Kilosa-Gulwe-Igandu, kutoa msaada wa kiutendaji na wa kitaasisi, na kusaidia uwezo wa mwitikio dhidi ya dharura, imesema taarifa hiyo.

Imesema mradi huo unatarajiwa kunufaisha moja kwa moja watu karibu 900,000 na kunufaisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja watu takribani milioni 3.5, sawa na asilimia tano ya watu wote wa Tanzania. Hii ni pamoja na watumiaji wa reli, wakazi wa kando ya njia hiyo ya reli, wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara na jamii katika eneo linalozunguka eneo la Kinywasungwe, imesema taarifa hiyo.

"Wakati mtandao wa usafirishaji nchini humo ni mpana, kuna vikwazo vinavyoendelea katika suala la ukarabati na uwezo ambavyo vinapunguza matumizi yake kamili," amesema Nathan Belete, mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa nchi za Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe.

"Uwekezaji huu utashughulikia moja kwa moja vikwazo katika mtandao wa reli ili kuboresha ufanisi, uwezo na ushindani ili kutumia kikamilifu fursa ya kipekee ya kijiografia ya Tanzania katika kuwezesha muunganisho wa kikanda," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha