China na Uganda zatafuta kwa pamoja maendeleo ya pande zote, asema Balozi wa China nchini Uganda

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 01, 2024

Zhang Lizhong (Kati), Balozi wa China nchini Uganda, akitoa maelezo kwa waandishi wa habari na washauri bingwa mjini Kampala, Uganda, Machi 28, 2024. (Xinhua/Nie Zuguo)

Zhang Lizhong (Kati), Balozi wa China nchini Uganda, akitoa maelezo kwa waandishi wa habari na washauri bingwa mjini Kampala, Uganda, Machi 28, 2024. (Xinhua/Nie Zuguo)

KAMPALA - Wakati ambapo China inaendelea kufuata ujenzi wa mambo yake ya kisasa, imedhamiria kushirikiana na mataifa mengine kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja, Zhang Lizhong, Balozi wa China nchini Uganda amesema mwishoni mwa wiki na kuongeza kuwa China imekuwa ikiunga mkono maendeleo ya Uganda katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na biashara, afya na kilimo, katika miongo sita iliyopita.

Zhang wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari na washauri bingwa katika Ubalozi wa China mjini Kampala, mji mkuu wa Uganda amesema kwamba ndani ya mifumo ya Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), China na Uganda zinafanya kazi kuelekea ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote ili kufikia maendeleo ya pamoja.

Chini ya BRI, China imefadhili na kujenga mitambo miwili ya kuzalisha umeme kwa maji, mtambo wa kuzalisha umeme kwa maji wa Bwawa la Karuma na Kituo cha Kuzalisha umeme kwa Maji cha Isimba, ambayo ni muhimu katika kushughulikia mahitaji ya Uganda yanayoongezeka ya nishati, na kuwezesha maendeleo yake ya viwanda.

Amesema, mbali na kusaidia maendeleo ya miundombinu ya nishati, China imeisaidia Uganda kuimarisha muunganisho wake na Dunia kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe, ambao umepanuliwa ili kukabiliana na ongezeko la abiria na mizigo. Na kwamba China imekuwa na mchango muhimu katika ujenzi wa Barabara ya Entebbe-Kampala, ikipunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kusafiri kati ya Kampala na Entebbe kwa nusu.

“Ujenzi wa miundombinu hii mikubwa ya nishati na usafiri siyo tu umetoa fursa za ajira lakini pia umewezesha uhamishaji wa ujuzi na maarifa” amesema Zhang huku akieleza kuwa maelfu ya watu wa Uganda walipata kazi, na wengine sasa wanajishughulisha na biashara za kibinafsi baada ya kupata ujuzi kutoka kwenye miradi hiyo.

Balozi huyo amesema, biashara ya pande mbili inaendelea kukua kwa kasi ambapo nchi hizo mbili zimeshuhudia ongezeko la biashara kwa miaka saba mfululizo. Amesema, miaka kumi iliyopita, thamani ya biashara ya pande mbili ilikuwa dola za Kimarekani karibu milioni 600 na kufikia mwisho wa 2023, iliongezeka hadi dola bilioni 1.3, ambapo mauzo ya Uganda kwenda China yameongezeka kwa asilimia 19 hadi kufikia dola milioni 70.

"China imeazimia kufungua mlango wa soko lake kwa upana zaidi kwa bidhaa bora za Uganda," Zhang amesema.

Amesema kuwa wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China mwezi Novemba mwaka jana, kampuni za Uganda zilitia saini mikataba ya kuuza tani 30 za kahawa iliyochomwa na makontena mengine 29 ya maharagwe ya kijani ya kahawa kwa wenzao wa China.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha