Mkoa wa Jiangsu wazamiria kuendeleza nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 03, 2024

Picha hii iliyopigwa tarehe 28 Februari 2024 ikionyesha mikono ya roboti ikifanya kazi katika karakana ya teknolojia za akili bandia huko Wuxi, Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China. (Xinhua/Ji Chunpeng)

Picha hii iliyopigwa tarehe 28 Februari 2024 ikionyesha mikono ya roboti ikifanya kazi katika karakana ya teknolojia za akili bandia huko Wuxi, Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China. (Xinhua/Ji Chunpeng)

BEIJING – Mkoa wa Jiangsu wa Mashariki ya China ambao ni mkoa wenye nguvu kubwa za kiuchumi nchini humo umeahidi kufanya juhudi zaidi za kuendeleza nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora mwaka huu, kwa malengo ya kujenga maabara mpya za kitaifa na kukuza kampuni zaidi za teknolojia.

Xu Kunlin, Mkuu wa Mkoa wa Jiangsu, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumanne kwamba juhudi zaidi zitafanywa ili kuongeza utafiti wa kimsingi, uboreshaji wa viwanda, na uvumbuzi wa biashara.

Xu amesema mkoa huo umetenga yuan jumla ya bilioni 2.48 (kama dola milioni 350 za Kimarekani) kwa ajili ya utafiti wa kimsingi mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kuboresha maabara na kuendeleza miradi kuu ya utafiti. Amesema, lengo moja ni kuongeza idadi ya maabara za kitaifa zinazoongozwa na mkoa huo hadi kufikia zaidi ya 40 kutoka 35 za sasa.

Kwa upande wa uboreshaji wa viwanda, Xu amesema juhudi zaidi zitachukuliwa ili kuendeleza viwanda vinavyoibukia kimkakati na kujenga mifumo ya viwanda ya siku za baadaye, na pia kuifanya sekta ya viwanda kuwa ya kisasa zaidi, ya kidijitali na iliyounganishwa kwenye mtandao wa intaneti.

Xu ametoa mfano wa kampuni ya kijadi iliyoboreshwa katika Mji wa Suzhou ambapo kupitia mageuzi ya teknolojia za akili bandia, karakana ya kielelezo ya kampuni hiyo imeboresha kiwango chake cha otomatiki hadi zaidi ya asilimia 90, ikipunguza mzunguko wa uzalishaji na uwasilishaji wa bidhaa kutoka siku saba hadi nusu siku, na kuongeza uwezo wa uzalishaji kwa zaidi ya mara mbili kwa kila bidhaa.

Xu amesema mkoa huo pia unalenga kuongeza idadi ya kampuni za teknolojia ya hali ya juu na kampuni ndogo na za kati za teknolojia hadi 55,000 na 100,000 mtawalia, mwaka huu.

“Jiangsu itaanzisha sera kadhaa mpya za kujenga mfumo wa uvumbuzi unaoongozwa na kampuni ambao unajumuisha mafungamano ya pande zote na kampuni, vyuo vikuu na taasisi za utafiti,” Xu amesema.

Mkoa huo ulishuhudia pato lake likiongezeka kwa asilimia 5.8 mwaka hadi mwaka na kufikia yuan trilioni 12.82 Mwaka 2023, ambao unachukua nafasi ya pili kote nchini China, ikiwa ni chini tu kidogo kwa lile la Mkoa wa Guangdong, Kusini mwa China.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha