Kampuni ya China yaanza ujenzi wa uwanja wa kisasa wa soka Kaskazini mwa Tanzania kwa ajili ya fainali za AFCON 2027

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 08, 2024

ARUSHA, Tanzania - Kampuni ya Uhandisi wa Ujenzi wa Reli ya China (CRCEG) imeanza ujenzi wa uwanja wa kisasa wa soka katika Jiji la Arusha, Kaskazini mwa Tanzania siku ya Jumamosi kwa ajili ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwenye mradi huo ilifanyika kwenye ardhi yenye ukubwa wa hekta 14.57, ambapo viongozi waandamizi wa serikali ya Tanzania waliungana na wahandisi na mafundi wa CRCEG kuanza kujenga uwanja huo ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Damas Ndumbaro amesema ujenzi wa uwanja huo wa kisasa ni hatua muhimu wakati ampapo Tanzania inajiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za AFCON pamoja na Kenya na Uganda.

Ndumbaro amesema uwanja huo wa Arusha umechukuliwa kuwa uwanja muhimu zaidi na wa kisasa zaidi unaojengwa na kampuni ya China nchini Tanzania katika miaka 20 iliyopita baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo katika mji wa bandari wa Dar es Salaam wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000.

“Huu ni muundombinu muhimu kwa Tanzania wakati nchi inajiandaa fainali za AFCON 2027 kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la Afrika na itajenga upya Sura ya Tanzania barani Afrika,” amesema Ndumbaro.

Gao Hongchun, meneja wa mradi huo, amesema mkandarasi ataweka mkazo katika kujenga moja ya viwanja bora zaidi barani Afrika, kutoa nafasi za ajira kwa wenyeji, kuhimiza ujenzi wa mijini, na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa kikanda.

Gao amesema mradi huo wa uwanja wa Arusha ni jengo jingine la alama la CRCEG baada ya kufanya kazi kwa bidii kwa zaidi ya miaka 20 katika soko la Arusha, baada ya miradi zaidi ya 10 ikiwa ni pamoja na makao makuu ya Kamisheni ya Nguvu za Atomiki ya Tanzania, jengo la kibiashara la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa Tanzania, na Hoteli ya Melia ya Arusha.

Machi 19, CRCEG ilisaini makubaliano na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Tanzania kujenga Uwanja huo wa Arusha.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha