

Lugha Nyingine
Watoto watatu wa kiongozi wa Kundi la Hamas Ismail Haniyeh wauawa katika shambulizi la Israel
GAZA - Watoto watatu wa Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Siasa ya Kundi la Hamas, pamoja na wajukuu zake watatu, wameuawa kwenye shambulizi la anga la Israel katika Mji wa Gaza siku ya Jumatano.
Ofisi ya vyombo vya habari ya Kundi la Hamas imeripoti kwamba watoto hao wameuawa katika shambulizi ndani ya gari lao walipokuwa wakiendesha katika kambi ya wakimbizi ya Al-Shati, Magharibi mwa Mji wa Gaza. Wajukuu watatu wa Haniyeh pia wameuawa katika shambulizi hilo.
Baadaye siku hiyo, Israel ilithibitisha rasmi shambulizi hilo.
"Ndege ilishambulia askari watatu wa Kundi la Hamas waliofanya shughuli za kigaidi katikati mwa Ukanda wa Gaza," idara ya usalama ya Israel ya Shin Bet na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) zimesema katika taarifa ya pamoja.
Taarifa hiyo inasema, watu hao watatu waliouawa ni Amir Haniyeh, Mohammad Haniyeh, na Hazem Haniyeh.
IDF imeongeza katika taarifa hiyo kwamba "inapata habari kwamba ndugu wengine wa Haniyeh wamejeruhiwa, miongoni mwao akiwemo mtoto mdogo. Lakini haijathibitishwa na IDF."
Haniyeh amesema katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Al Jazeera baada ya shambulio hilo kwamba kuuawa kwa wanawe hakutaathiri masharti ya Hamas katika mazungumzo ya kusimamisha mapigano Gaza.
Haniyeh, kiongozi wa Kundi la Hamas mwenye umri wa miaka 61, anaishi Qatar.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma