Maonyesho ya Soko la Utalii Duniani la Afrika mwaka 2024 lafunguliwa Afrika Kusini

(CRI Online) April 11, 2024

Maonyesho ya 10 ya Soko la Utalii Duniani mwaka 2024 yameanza jana Jumatano mjini Cape Town, Afrika Kusini, na kukutanisha watu maarufu katika sekta ya usafiri na utalii kwa lengo la kujadili fursa za biashara katika sekta ya utalii.

Maonyesho hayo yanayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Cape Town, yanaonyesha umuhimu wa fursa za utalii katika kanda hiyo kupitia mfululizo wa burudani, mikutano, na hafla za utoaji wa tuzo.

Waandalizi wa maonyesho hayo wamesema, yakiwa ni sehemu ya Wiki ya Usafiri ya Afrika 2024 iliyoanza tarehe 7 hadi 12 mwezi huu mjini Cape Town, maonyesho hayo yameandaliwa ili kuboresha ufahamu wa sekta ya utalii, kuongeza mawasiliano, na kuboresha ukuaji wa biashara.

Pia maonyesho hayo yanatoa fursa kwa mashirika ya ndege, kampuni za meli za utalii, mahoteli na wakala wa usafiri kuonyesha huduma zao bora kwa jamii ya kimataifa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha