

Lugha Nyingine
Kutoka kujikimu hadi ustawi: Wakulima wadogo wa Kenya watumia teknolojia za kisasa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Picha ya kumbukumbu ikionyesha wakulima wa Kenya wakiponda mazao ya nyasi za Juncao katika shamba la Juncao lililoko Kijiji cha Lenginet, Nakuru, Kenya, Januari 26, 2024. (Xinhua/Han Xu)
NAKURU, Kenya - Kwa furaha tele, Pauline Mogambi, mkulima mdogo wa Kenya alikuwa akitazama kwa mshangao mboga za asili zinazochanua kwenye shamba lake katika Kaunti ya Nakuru, Kaskazini-Magharibi mwa Kenya, umbali wa takriban kilomita 180 kutoka mji mkuu Nairobi.
Mama huyo wa watoto wawili ni mmoja wa watumiaji wa mapema wa kilimo cha jadi, ambacho kinaendeleza rutuba ya udongo kwa njia ya kulima kidogo pamoja na mbinu zisizo na kemikali za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao na magonjwa ili kuongeza mavuno.
Tangu alipoanza kulima kilimo cha bila kulima, kupanda mazao mchanganyiko kwa pamoja na kuweka mbolea ya samadi, shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja limezalisha mazao ya kutosha kulisha familia yake na kuuza ziada katika masoko ya kaunti hiyo.
"Nimekuwa mkulima kwa miongo miwili na nilikuwa nikipata mavuno madogo, lakini nilipotumia kilimo ya jadi na mbinu zisizo na kemikali za kudhibiti magugu na wadudu, mavuno ya jumla yameongezeka," Mogambi ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua akiwa kwenye shamba lake siku ya Jumatatu.
Wakulima wadogo katika Kaunti ya Nakuru, mojawapo ya maeneo yanayozalisha mazao ya chakula kwa wingi nchini Kenya, hawajaepushwa na changamoto zinazoletwa na kuongezeka kwa joto la sayari ya Dunia, ikiwa ni pamoja na wadudu waharibifu, magonjwa, kuyumba kwa soko na kupungua kwa ardhi ya kilimo.
Shirika la Washauri wa Utafiti wa Kilimo wa Kimataifa (CGIAR), kupitia Mpango wake wa Kulima Mazao Mchanganyiko wa Mashariki na Kusini mwa Afrika, hata hivyo limesaidia wakulima hao katika kutumia teknolojia na ubunifu unaoimarisha uwezo wao wa kukabilianana mabadiliko ya tabianchi, kuendeleza usalama wa chakula na lishe.
Nchini Kenya, mpango huo uliopewa jina la "Ukama Ustawi," unatekelezwa huko Nakuru na kaunti za mashariki mwa Kenya za Embu na Makueni.
Shamba la Mogambi limetumika kama eneo la kielelezo kwa mbinu mbalimbali zenye uvumbuzi, ikiwa ni pamoja na kilimo cha bila kulima, kung'oa, kupanda mazao mchanganyiko kwa pamoja, na kupanda mazao kwa mzunguko au kupokezana na kilimo cha misitu.
Tangu atumie mbinu hizi za kilimo cha teknolojia za kisasa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Mogambi amepata ongezeko mara tatu la mavuno ya mahindi, kunde, kale, viazi vitamu na matunda, huku akiboresha lishe na mapato ya familia yake.
Mpango wa "Ukama Ustawi" unaotekelezwa katika nchi 12 za Afrika, ikiwemo Kenya, umeimarisha mavuno wa wakulima wadogo, na kuongeza mapambano dhidi ya njaa na umaskini vijijini, amesema Said Boaz Waswa, mwanasayansi wa udongo wa Muungano wa Kimataifa wa Bioanuai na Kituo cha Kimataifa cha Kilimo cha Kitropiki (CIAT).
Picha ya kumbukumbu ikionyesha wafanyabiashara wakipima pilipili hoho kwenye soko la Makutano katika Kaunti ya Kirinyaga, Kenya, Julai 17, 2023. (Picha na John Okoyo/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma