

Lugha Nyingine
Mashindano ya Tuzo ya pili ya mawasiliano ya kimataifa ya "Njia ya Hariri" yaanza kukusanya kazi
Mashindano ya Tuzo ya pili ya Mawasiliano ya Kimataifa ya “Njia ya Hariri” yameanza rasmi kukusanya kazi za kushiriki siku ya Ijumaa chini ya maandalizi ya Shirikisho la Ushirikiano wa Habari la "Ukanda Mmoja, Njia Moja" na uongozi wa gazeti la People's Daily, ambalo ni shirika mwenyekiti wa shirikisho hilo.
Tuzo ya Mawasiliano ya Kimataifa ya "Njia ya Hariri" ni shughuli muhimu ya Shirikisho la Ushirikiano wa Habari la "Ukanda Mmoja, Njia Moja" (BRI). Inalenga kuhimiza moyo wa Njia ya Hariri wa amani na ushirikiano, uwazi na ujumuishaji, kufundishana, na kunufaishana na manufaa kwa pande zote.
Lengo lake ni kuhamasisha na kuongoza vyombo vya habari vya nchi na maeneo yanayojenga pamoja "Ukanda Mmoja, Njia Moja" kujifunza kutoka kwa kila mmoja, na kusimulia pamoja simulizi za "Ukanda Mmoja, Njia Moja".
Kuna kategoria nne za tuzo kwenye mashindano hayo: Tuzo ya Ripoti Bora, Tuzo ya Picha Bora, Tuzo ya Video Bora, na Tuzo ya Uvumbuzi Bora. Kwa kila kategoria kutakuwa na tuzo kuu moja, tuzo nne za wateuliwa, na tuzo kumi za wale watakaoingia fainali.
Kazi zote zinazounga mkono pendekezo la kujenga pamoja "Ukanda Mmoja, Njia Moja", kuwasilisha moyo wa "Njia ya Hariri", kuonyesha mabadilishano na kufundishana kati ya ustaarabu mbalimbali, kuendana na dhana ya kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja wa binadamu na zina mchango mkubwa katika mawasiliano ya kimataifa zinaweza kushiriki kwenye mashindano.
Kazi zitakazoshiriki lazima ziwe zile zilizotengenezwa na upande wa nje ya China, au kutengenezwa chini ya ushirikiano wa upande wa China na wa nchi nyingine, au ziwe zimetengenezwa na upande wa China na kutangazwa kwenye majukwaa ya nchi nyingine.
Washiriki lazima wawe wamejisajili kwenye tovuti rasmi ya Shirikisho la Ushirikiano wa Habari la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” (www.brnn.com) na kutuma taarifa husika za kazi zao.
Uteuzi wa kazi zitakazoshiriki kwenye mashindano hayo, umegawanyika katika raundi mbili: tathmini ya awali itakayofanywa na kamati ya wanataaluma na tathmini ya mwisho itakayofanywa na kamati ya ukaguzi. Matokeo yatachapishwa mara moja baada ya uteuzi kwenye tovuti hiyo.
Kuanzia Januari 2020 hadi Septemba 2021, Mashindano ya Tuzo ya kwanza ya "Njia ya Hariri" yalifanya ukusanyaji wa kazi, ambao ulikamilika Desemba 2022, na shughuli za kutunukia tuzo washindi zilifanyika mwaka 2023. Kazi 19 ikiwemo "Kazakhstan na Pendekezo la BRI: Mwelekeo ni Upi?" zilishinda kategoria tano za tuzo kama vile Tuzo ya Ripoti za Kina, na mkuu wa Klabu ya “Marafiki wa BRI” wa Pakistan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasomi wa Pakistan-China Mushahid Hussain Sayed alishinda Tuzo ya Mchango Maalum.
Shirikisho la Ushirikiano wa Habari la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ni jukwaa la ushirikiano linaloundwa na vyombo vya habari vya nchi na maeneo yanayojenga pamoja pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”. Linalenga kusaidia vyombo hivyo kuimarisha uelewano, kuongeza urafiki, kuhimiza ushirikiano, na kuwa na mfumo wa kawaida wa uratibu. Hadi kufikia sasa shirikisho hilo limevutia vyombo vya habari 261 kutoka nchi 109 kuwa sehemu yake.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma