China yatoa yuan zaidi ya bilioni 200 kutoka bajeti ya serikali kuu kwa ajili ya uwekezaji

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 18, 2024

BEIJING - Yuan zaidi ya bilioni 200 (kama dola bilioni 28.16 za Kimarekani) za bajeti ya serikali kuu ya China zimetolewa hadi kufikia sasa kwa mwaka huu ili kupanua uwekezaji, Liu Sushe, naibu mkuu wa Kamati ya Kitaifa ya Maendeleo na Mageuzi ya Kina ya China amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano.

“Fedha hizo zilizotolewa zinachukua asilimia zaidi ya 30 ya kiasi kilichopangwa kwa mwaka” Liu amesema, huku akiongeza kuwa kamati hiyo itaharakisha kugawanya fedha husika, kuimarisha usimamizi wa miradi, na kuboresha ufanisi wa matumizi ya fedha hizo za bajeti ya serikali kuu.

Yuan jumla ya bilioni 700 zitatengwa kutoka kwenye bajeti ya serikali kuu kwa ajili ya uwekezaji Mwaka 2024, kwa mujibu wa ripoti ya kazi ya serikali ya China ya mwaka huu.

Licha ya fedha za bajeti ya serikali kuu, China pia inapanga kutoa yuan trilioni 3.9 za dhamana maalum kwa serikali za mitaa, ikiwa ni ongezeko la yuan bilioni 100 kutoka kwenye kiwango cha mwaka jana.

“Kamati imekamilisha uteuzi wa awali wa miradi ya dhamana maalum ya serikali za mitaa” Liu amesema, akiongeza kuwa kundi hili lina miradi ya kutosha na mahitaji makubwa ya mtaji, likiweka msingi thabiti wa utoaji na matumizi ya hati fungani za serikali za mitaa.

Juhudi pia zimefanywa kuendeleza utekelezaji wa miradi inayoungwa mkono na dhamana ya hazina ya Yuan trilioni 1 iliyotengwa Mwaka 2023, Liu amesema.

Ameongeza kuwa kamati hiyo imetenga fedha hizo kwa ajili ya miradi 15,000 na itahimiza miradi hiyo kuanza kutekelezwa kabla ya mwisho wa Mwezi Juni mwaka huu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha