China yawatunuku medali wanaanga wa chombo cha Shenzhou-16

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 19, 2024

BEIJING - Wanaanga watatu walioshiriki kwenye safari ya chombo cha Shenzhou-16 kwenye anga ya juu wametunukiwa medali siku ya Alhamisi kutokana na mchango waliotoa kwa ajili ya mambo ya China ya safari kwenye anga ya juu. Jing Haipeng ametunukiwa medali ya ngazi maalum ya mafanikio ya safari kwenye anga ya juu. Zhu Yangzhu na Gui Haichao wamepokea medali za daraja la tatu za mafanikio ya safari kwenye anga ya juu na kupata sifa ya heshima ya "Mwanaanga Mashujaa."

Tuzo hizo zimetolewa na Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Baraza la Serikali la China na Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC).

Jing ameshiriki mara nne safari za chombo kwenye anga ya juu na kufanya kazi ya kuwa kiongozi mara tatu wa kutekeleza jukumu la safari ya chombo kwenye anga ya juu. Na amekuwa mwanaanga wa China aliyeshiriki mara nyingi zaidi jukumu la chombo kinachobeba binadamu kwenye safari ya anga ya juu.

Zhu ni mhandisi wa kwanza wa China wa kutekeleza safari kwenye anga ya juu kwa kupanda chombo cha kubeba binadamu na kufanya shughuli nje ya chombo kwenye anga ya juu. Gui ni mtaalamu wa kwanza wa China wa kushughulikia mizigo inayobebwa kwenye chombo cha kubeba binadamu kufanya safari kwenye anga ya juu.

Kikiwa kilirushwa Mei 30, 2023, chombo cha safari kwenye anga ya juu cha Shenzhou-16 kiliwapeleka wanaanga hao watatu kwenye moduli ya msingi ya kituo cha anga ya juu cha China cha Tianhe, ambapo waliishi na kufanya kazi kwa miezi mitano kwenye kituo hicho.

Wakati wa kuwepo kwao kwenye kituo hicho cha anga ya juu, walifanya shughuli nje ya chombo kwa mara moja, kufanya kazi ya kutangaza moja kwa moja shughuli zao kutoka kituo cha anga ya juu kwa dunia, na kufanya mfululizo wa majaribio kwenye anga ya juu wakiwa kwenye obiti.

Wanaanga hao watatu walirejea duniani salama Oktoba 31, 2023. Chombo cha Shenzhou-16 kilitekeleza jukumu la kwanza la kubeba binadamu kwenye safari ya anga ya juu katika wakati wa kipindi cha matumizi na maendeleo ya kituo cha anga ya juu cha China. Pia ni mara ya kwanza kwa aina tatu za wanaanga -- rubani, mhandisi wa chombo na mtaalamu wa kushughulikia mizigo iliyopakiwa -- kutekeleza pamoja jukumu la chombo cha safari kwenye anga ya juu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha