Rais wa Kenya athibitisha kifo cha mkuu wa majeshi ya Kenya katika ajali ya ndege

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 19, 2024

NAIROBI - Rais wa Kenya William Ruto amethibitisha kwamba mkuu wa majeshi ya nchi hiyo Francis Ogolla ni miongoni mwa makamanda waandamizi 10 waliofariki katika ajali ya helikopta iliyotokea eneo la kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo jana, siku ya Alhamisi.

Rais Ruto amesema Ogolla, mkuu wa Vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), alikuwa ndani ya helikopta aina ya Huey ya jeshi hilo na wanajeshi wengine 11. Amesema, helikopta hiyo ilipaa kutoka shule moja ya msingi katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet kabla ya kuanguka na kuwaka moto majira ya saa 8:20 mchana kwa saa za Kenya (1120 GMT).

Akizungumza katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja kupitia televisheni katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Rais Ruto amesema kuwa maafisa 10 wa kijeshi, akiwemo Ogolla, wamefariki katika ajali hiyo, huku wengine wawili wakinusurika na sasa wamelazwa hospitalini. "Huu ni wakati wa huzuni kubwa," ameongeza.

Amesema kuwa Ogolla aliondoka Nairobi asubuhi kuzuru wanajeshi waliotumwa katika eneo hilo lenye matatizo ili kupambana na majambazi na kukagua kazi inayoendelea ya ukarabati wa shule.

“Kikosi cha Jeshi la Anga la Kenya kimeunda na kutuma timu ya uchunguzi wa anga ili kubaini chanzo cha ajali hiyo” Rais Ruto amesema.

Pia ametangaza kuwa nchi hiyo itatenga muda wa maombolezo wa siku tatu kuanzia leo Ijumaa ili kukumbuka maisha na taaluma ya kijeshi ya jenerali huyo aliyefariki, ambaye si tu amepoteza maisha yake akiwa madarakani bali pia akiwa katika kazi za kijeshi.

Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema kuwa helikopta hiyo ya KDF ilianguka umbali wa kilomita mbili na kuwaka moto muda mfupi tu baada ya kupaa kutoka eneo la mpaka wa Elgeyo Marakwet-Pokot Magharibi.

"Tuliona helikopta hiyo ikianguka, na tulipokimbilia eneo la tukio, tulikuta helikopta ikiwa inawaka moto," amesema Evans Kipkosgei, mkazi wa eneo hilo, huku akiongeza kuwa eneo hilo lilizingirwa mara moja na maafisa wa KDF walioko Bonde la Kerio.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Rais Ruto kufuatia kifo cha Ogolla. "Natuma salamu zangu za rambirambi kwa amiri jeshi mkuu wa Vikosi vya Jeshi la Kenya, Rais William Ruto, Wakenya wote, familia, jamaa na marafiki wa wote waliopoteza maisha katika ajali hiyo," ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, ambao zamani uliitwa Twitter. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha