Huawei kuboresha mtandao wa mawasiliano kwa kaya za kipato cha chini nchini Kenya

(CRI Online) April 23, 2024

Kampuni ya teknolojia ya Huawei ya China, imesema Jumatatu kwamba inaongeza kasi ya kusambaza miundombinu ya mtandao wa mawasiliano kwa kaya zenye kipato cha chini nchini Kenya ili kuendeleza uchumi wa kidijitali nchini humo.

Akiongea kando ya Mkutano wa 'Afrika iliyounganishwa wa 2024', unaofanyika mjini Nairobi chini ya kaulimbiu ya "Kuunda Mustakabali wa Afrika Iliyounganishwa: Kufungua Ukuaji Zaidi ya Muunganisho", Mkurugenzi wa masuala ya serikali na ushirikiano wa Huawei nchini Kenya, Adam Lane, amesema kwamba nyumba nyingi za kiwango cha juu zina chaguo la kuunganishwa na mtandao wa mawasiliano, ukiwemo mkonga wa mawasiliano, tofauti na makazi ya watu wa kipato cha chini.

Amebainisha kuwa kampuni hiyo ina teknolojia mahususi kwa ajili ya kaya zenye kipato cha chini ambazo zinarahisisha kuunganishwa kwa mtandao wa mawasiliano na kutumia vifaa vichache, jambo ambalo husaidia kupunguza gharama na kuongeza kasi ya upatikanaji wa intaneti.

Mkutano huo wa siku tano umewaleta pamoja mawaziri na wadhibiti wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kutoka nchi 35 za Afrika, pamoja na maafisa wa Umoja wa Ulaya, ili kutafuta njia za kupunguza pengo la kidijitali barani Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha