Kenya yaendeleza usafiri wa kijani kwa kutumia teknolojia ya magari yanayotumia umeme ya China

(CRI Online) April 24, 2024

Wataalamu wa teknolojia wamepongeza teknolojia ya magari yanayotumia umeme ya China siku ya Jumanne wakati ambao Wakenya wanaendelea kukumbatia njia za kijani za usafiri.

Akizungumza kwenye mkutano wa pili wa Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Kenya, Kenya Power kuhusu magari yanayotumia umeme, uliofanyika mjini Nairobi nchini Kenya, katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Petroli ya Kenya, Alex Wachira amesema magari yanayotumia umeme ya China yameibuka kuwa njia mbadala ya magari ya jadi yanayotumia mafuta.

Amezipongeza kampuni zote za China zinazoendesha shughuli za kuunganisha sehemu za magari nchini Kenya kwa sababu zimechukua jukumu katika kuongeza matumizi ya magari yanayotumia umeme nchini humo.

Mkutano huo wa siku mbili umewaleta pamoja wajumbe zaidi ya 200, wakiwemo maafisa wa serikali, wafadhili, na wataalam wa magari yanayotumia umeme kutoka kote duniani, ili kutafuta suluhu za kiubunifu na za kimageuzi za kuondoa kaboni katika sekta ya uchukuzi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha