China yakanusha shutuma za Marekani kuhusu mawasiliano ya kawaida kati ya China na Russia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 24, 2024

BEIJING - China inakanusha vikali shutuma zisizo na msingi za Marekani juu ya mawasiliano ya kawaida ya kibiashara na kiuchumi kati yake na Russia, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin amesema siku ya Jumanne kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Marekani inaendelea kutoa shutuma zisizo na msingi juu ya mawasiliano ya kawaida ya kibiashara na kiuchumi kati ya China na Russia, huku ikipitisha mswada wa kutoa msaada mkubwa kwa Ukraine, Wang amesema kwenye mkutano huo alipoulizwa kuhusu shutuma za Marekani na vikwazo vinavyowezekana kuhusu suala hilo.

"Kuwasha moto huku ikielekeza lawama kwa wengine, huu ni unafiki na kutowajibika sana. China inapinga vikali," amesema.

Wang amesema kuhusu suala la Ukraine, msimamo wa China siku zote umekuwa wa haki na usiopendelea. Amesema, China imefanya jitihada za kuhimiza mazungumzo ya amani na suluhu ya kisiasa na kwamba Serikali ya China inadhibiti usafirishaji wa bidhaa za matumizi ya namna mbili kwa mujibu wa sheria na kanuni.

"China siyo mwanzilishi wa mgogoro wa Ukraine wala siyo sehemu yake. Hatujawaji kamwe kuchochea moto huo au kutafuta maslahi ya binafsi, na kwa hakika hatutakubali kuwa mbuzi wa kafara," Wang amesema.

Amesisitiza tena kwamba juu ya msingi wa usawa na kunufaishana, haki ya China ya kufanya mawasiliano ya kawaida ya kibiashara na kiuchumi na Russia na nchi nyingine haipaswi kuingiliwa au kuvurugwa. "Haki na maslahi halali na ya kisheria ya China hayapaswi kukiukwa."

“Kuchochea moto au kupaka matope wengine siyo utatuzi sahihi wa suala la Ukraine,” Wang amesema, huku akiongeza kuwa kushughulikia tu masuala halali ya usalama ya pande zote na kuunda mfumo wa usalama wa Ulaya ulio na uwiano, wenye ufanisi na endelevu kupitia mazungumzo na majadiliano ndio njia sahihi ya kusukuma mbele kwa kutatua mgogoro huo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha